Makamu Mwenyekiti wa Kikundi cha Tanzania One Movement Wilayani Nyasa Bw Onesmo
Mkandawile hivi karibuni, akikabidhi vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa CORONA vyenye
Thamani ya tsh 116,000/= kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba ili, avigawe kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa. Makabidhiano hayo yamefanyika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa(picha na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Nyasa)
……………………………………………………………………………………………
Kikundi cha Tanzania One Movement Wilaya ya Nyasa,hivi karibuni kimetoa msaada wa vifaa vya kunawia maji vyenye Thamani Ya Tsh 116,000/ kwa Wananchi wa Wilaya ya Nyasa ili kujikinga na Virusi vya Corona .
Vifaa hivyo vimekabidhiwa hivi karibuni na Makamu Mwenyekiti Wilayani Nyasa, Bw Onesmo Mkandawile kwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba ili, avigawe kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa ili wachukue tahadhari, ya kukabiliana na Ugonjwa wa Corona kwa kunawa mikono .
Akikabidhi vifaa hivyo Bw. Mkandawile alifafanua kuwa wao kama wanakikundi wameamua kuchanga fedha hizo hizo kuto mifukoni mwao na kuunga juhudi za Serikali za kupambana na Ugonjwa wa Corona ambao hauna kinga wala dawa.
Alivitaja vifaa alivyochangia kuwa ni, Ndoo (4) na mifuniko yake za kunawia maji tiririka , na sabuni za nusu lita kopo 05, tishu bunda 04. Aidha alitoa wito kwa wananchi wote wa Wilaya ya Nyasa, kufuata maelekezo ya wataalamu wa Afya pamoja na Viongozi wa Serikali, ili waweze kujikinga na Ugonjwa wa Corona.
Akipokea Msaada huo kwa niaba ya Wananchi wa Wilaya ya Nyasa,Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Bi Isabela Chilumba, amewashukuru wanakikundi hao kwa kutoa Msaada kwa wananchi wa Wilaya ya Nyasa, kwa kuwa ni Msaada ambao ulikuwa ukihitajika, na wanakikundi hao wameonyesha nia ya kuisaidia jamii katika mapambano ya ugonjwa huu wa Corona, hivyo aliwataka wananchi wa Wilaya ya Nyasa kuhakikisha wanakuwa na sehemu nyingi za kunawa mikono, ili kujikinga na Ugonjwa wa Corona. Aidha alizitaka jamii zingine kuiga mfano wa wanakikundi hao na kuwaagiza watoe elimu ya kupambana na ugonjwa wa CORONA kwa Wananchi wengine.