Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma
Benki ya Ushirika Tanzania (Cooperative Bank Tanzania Plc) imefanya Mkutano Mkuu wa Pili wa Wanahisa jijini Dodoma, ukiwakutanisha wanahisa, wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, viongozi wa benki pamoja na wadau mbalimbali kujadili maendeleo ya benki hiyo na mwelekeo wake wa ukuaji.
Mkutano huo uliofanyika Julai 31, 2026, ulitoa fursa kwa wanahisa kupitia na kujadili utendaji wa benki kwa mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2025.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Coop Bank Tanzania Plc, Godfrey Ng’urah amesema benki hiyo imeendelea kukua kwa kuongeza mikopo, amana, mtaji pamoja na kuboresha huduma za kidigitali.
Amesema mikopo ya benki hiyo imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 14 mwaka 2024 hadi kufikia Shilingi bilioni 102 mwaka 2025, jambo ambalo limewezesha kuwahudumia wanachama, wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara, wajasiriamali na vyama vya ushirika.
Amebainisha kuwa amana za benki zimeongezeka kutoka Shilingi bilioni 15 hadi kufikia Shilingi bilioni 114, huku mtaji wa fedha za wanahisa ukiongezeka kutoka Shilingi bilioni 27 wakati wa kuunganisha benki mbili hadi kufikia Shilingi bilioni 42.
Ameongeza kuwa benki hiyo imefanya mageuzi makubwa ya kidigitali kwa kuanzisha huduma mbalimbali ikiwemo Kopo Wakala, Kopo Pesa na COÖP Net.
Amesema kupitia Kopo Pesa, wateja wanaweza kufanya miamala mbalimbali kupitia simu za kiganjani ikiwemo kulipa LUKU, DSTV, maji na umeme pamoja na kutuma na kupokea fedha.
Aidha, amesema COÖP Net imewezesha vyama vikuu na taasisi kufanya malipo makubwa ikiwemo mishahara na malipo kwa wanachama zaidi ya 3,000 kwa wakati mmoja.
“Ni mwaka mkubwa, ni mwaka wa mageuzi, ni mwaka wa mafanikio. Tumejenga miundombinu imara na ya msingi kuhakikisha tunajenga benki kwa siku zijazo,” amesema Ng’urah.

Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Ushirika nchini Tanzania na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC), Dkt. Benson Ndiege amewataka wanahisa na wananchi kuendelea kuwekeza katika Benki hiyo.
Amesema hisa zilizokuwa zimekubalika wakati wa uzinduzi wa benki hiyo zilifikia Shilingi bilioni 58 na baada ya kukamilika kwa hatua hiyo kutakuwa na mpango mwingine wa kuongeza mtaji kupitia hisa.
Ameongeza kuwa fursa ya kuwekeza katika benki hiyo ipo kwa makundi mbalimbali kupitia vyama vya ushirika, ikiwemo waandishi wa habari, wavuvi, vijana na waendesha bodaboda.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema Benki ya Ushirika Tanzania inaweza kuwa miongoni mwa benki zinazokua kwa kasi kutokana na mipango yake ya maendeleo.
Amesema ndani ya muda mfupi benki hiyo imeonesha mabadiliko makubwa katika utoaji wa huduma kwa wateja.
“Ni muda mfupi mwaka mmoja lakini tunaona mabadiliko makubwa. Tunaona huduma nzuri sisi ambao tayari tumefungua akaunti kwenye benki hii,” amesema Senyamule.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA SACCOS, Mbogo Kerenge amesema ukuaji wa benki hiyo utawezesha vyama vya ushirika kupata mikopo kwa urahisi kutokana na kuongezeka kwa ukwasi.
Amesema vyama vya ushirika vinapaswa kuunganisha nguvu kwa kuchangia kulingana na uwezo wao ili kujenga benki yenye nguvu kama ilivyo kwa benki za ushirika katika nchi nyingine.
Ametoa mfano wa Benki ya Ushirika ya Kenya akisema imekuwa miongoni mwa benki kubwa katika sekta ya benki nchini humo, hivyo Tanzania nayo inaweza kufikia hatua hiyo kupitia ushirikiano wa vyama vya ushirika.

