Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (MB) (wa pili kushoto), akiwa katika mkutano wa kimkakati jijini London Uingereza na maafisa wakuu wa Citibank chini ya uongozi wa Afisa Mkuu Mtendaji anayesimamia eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akin Dawodu (wa tatu kulia), katika ziara yake rasmi ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha za kimataifa na wawekezaji, mkutano uliohudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini humo, Mhe. Mbelwa Kairuki (wa kwanza kushoto) na Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine (wa tatu kushoto)

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (MB) (kushoto), akisalimiana na Afisa Mkuu Mtendaji wa CitiBank, anayesimamia eneo la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akin Dawodu, katika ziara yake rasmi ya kiserikali kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha za kimataifa na wawekezaji, jijini London nchini Uingereza.

i(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha-London)

…………. 

Na Benny Mwaipaja, London

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mbunge), Julai 23, 2026 alifanya mkutano wa kimkakati jijini London na viongozi wa Citibank wakiongozwa na Mtendaji Mkuu wa Kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Akin Dawodu, ikiwa ni sehemu ya programu yake rasmi ya kuimarisha ushirikiano na taasisi za kifedha za kimataifa pamoja na wawekezaji.

Pande hizo mbili zilipitia historia ya ushirikiano wao wa muda mrefu tangu Citibank ilipoanza shughuli zake nchini Tanzania mwaka 1995, na kujadili masuala mbalimbali ikiwemo viwango vya ukadiriaji wa uwezo wa nchi kukopa (sovereign credit ratings), utoaji wa kwanza wa Hati Fungani ya Kimataifa (Eurobond), ufadhili kupitia taasisi za dhamana ya mikopo ya mauzo ya nje (Export Credit Agencies – ECAs), miradi ya miundombinu, mageuzi ya soko la mitaji na uhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi.

Mhe. Balozi Omar aliwapa viongozi wa Citibank taarifa kuhusu maendeleo ya hivi karibuni ya uchumi wa Tanzania, ikiwemo ongezeko kubwa la uwezo wa kuzalisha umeme, maboresho ya Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, pamoja na upanuzi wa miundombinu ya usafiri wa anga.

Aidha, aliwasilisha Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050, inayolenga kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa thamani ya dola za Marekani trilioni 1 katika kipindi cha miaka 25 ijayo, ambapo takribani asilimia 70 ya uwekezaji unaohitajika unatarajiwa kutoka sekta binafsi.

Waziri huyo pia aliieleza Citibank kuwa mazungumzo kuhusu mradi wa Gesi Asilia Iliyoyeyushwa (LNG) wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 42 yamekamilika kwa kiwango kikubwa, huku makubaliano kuhusu mfumo mkuu wa utekelezaji yakifikiwa. Alisema mradi huo unatarajiwa kuanza mara tu masuala yaliyosalia ndani ya muungano wa wawekezaji (consortium) yatakapokamilishwa.

Akizungumzia mageuzi ya kodi na mazingira ya biashara, Waziri Omar alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume mbili za Rais; moja ya kuboresha mazingira ya biashara na nyingine ya kufanya mapitio ya mfumo wa kodi. Alisema tume ya kodi imewasilisha mapendekezo 284 ambayo kwa sasa yanazingatiwa na Serikali.

Alisisitiza kuwa mageuzi yajayo yatalenga kupanua wigo wa walipakodi, kuboresha usimamizi wa kodi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, badala ya kuongeza mzigo wa kodi kwa walipakodi.

Kutokana na kupanuka kwa maeneo ya ushirikiano, Waziri Omar alipendekeza kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali ya Tanzania na Citibank, utakaohusisha masoko ya mitaji ya Serikali, ufadhili wa miradi ya miundombinu, ufadhili kupitia taasisi za dhamana ya mikopo ya mauzo ya nje (ECAs), mahusiano na wawekezaji, maendeleo ya soko la mitaji la ndani, uhamasishaji wa uwekezaji wa sekta binafsi pamoja na mageuzi ya usimamizi wa kodi.

Kwa upande wake, Citibank ilikaribisha pendekezo hilo na kuthibitisha dhamira yake ya kuendelea kuwa mshirika wa kimkakati wa muda mrefu wa Tanzania.