Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe.Dkt Riziki Pembe Juma, alikuwa Mgenirasmi katika Maadhimisho ya miaka 10 ya Tuzo ya Kiswahili ya “Safal ya Kiswahili ya Fasihi ya Afrika” iliyofanyika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar.es salaam Kampasi ya Mlimani Jijini Dar-es-salam.
Dar-es-salaam. 25.07.2026.
Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe.Dkt Riziki Pembe Juma amesema Serikali zote mbili za Tanzania, zinaendelea kuthamini na kuwekeza katika lugha ya Kiswahili.
Amesema lugha hiyo imekuwa rasmi na inatumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, SADC na Umoja wa Afrika ambapo inazidi kupata nafasi katika Taasisi mbalimbali za Kimataifa ikiwemo, UNESCO.
Dkt.Riziki ameyasema hayo wakati wa Maadhimisho ya miaka 10 ya Tuzo ya Kiswahili ya “Safal ya Kiswahili ya Fasihi ya Afrika” iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar.es salaam Kampasi ya Mlimani.
Amesema mafanikio hayo, yanahitaji kuendelezwa kwa kuzalisha kazi bora za fasihi ili kiswahili kiendelee kuwa lugha ya Elimu, Tafiti, Ubunifu na Diplomasia kama walivyosema wahenga “Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”.
Aidha, Dkt.Riziki, amewapongeza Washindi na Washiriki wa Tuzo hizo kwa Ujumla huku akiwaomba kuendelea kuandika na kutokata tamaa katika Uandishi ili wàendelee kupata tuzo ambazo zinatolewa kila mwaka.
Mbali na hayo, amewapongeza waandaji wa Tuzo hizo Kampuni ya ALAF, kwani wamekuwa ni wadau wakubwa wanaochangia kukieneza Kiswahili Kimataifa, huku akiwaomba kuweka fungu maalumu kwa walimu na wahadhiri wa Kiswahili ili kuwapa nguvu katika kazi yao hiyo.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Habri Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar Matar Zahor Masoud amesema lugha ya kiswahili ni Tunu ya Taifa na adhimu, hivyo Viongozi na Wananchi wanapaswa kuitunza na kuiendeleza ili isaidie katika kunyanyua Uchumi wa Nchi na Bara la Afrika kwa Ujumla.
Pia amewaomba Waandishi wa Fasihi na Wadhamini wa Tuzo hizi, wasiishie kwenye Tuzo pekee, bali waendelee kufanya tafakuri juu ya lugha hiyo kwa kuona maendeleo na changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa lengo la kukikuza Kiswahili Duniani.
Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Kampeni ya Alaf Limited, ilioandaa tunzo hizo bw.Bibhu Nanda amesema kiasi ya Dola 130,000 zimetumika kwa ajili ya kutoa zawadi kwa Washindi 40, tokea mwaka 2015 walipoanzisha.
Sambamba na hayo, amesema Makala zaidi ya 8000 zimenunuliwa na kusambazwa katika Vyuo Vikuu, Maktaba za Taifa, Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi za Tanzania na Kenya.
Tuzo hizo kwa mwaka 2026, zimeshirikisha mashindano ya Hadithi fupi fupi, Riwaya na Ushairi ambapo washindi wa kwanza kwa kila tunzo wamezawadiwa dola 5,000.

Imetolewa na Kitengo cha Habari, Mawasiliano na Uhusiano.WHSUM.
