Chakechake, Julai 24, 2026
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inashiriki Maonesho ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika Uwanja wa Gombani, Pemba, ambapo inaendelea kutoa elimu na huduma kuhusu utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa wananchi.
Katika maonesho hayo yanayovutia mamia ya wananchi, HESLB inashirikiana na maafisa kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kitengo cha Anwani za Makazi (NaPA) pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Miongoni mwa wanaotembelea banda la HESLB ni viongozi na wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu, ambao wanaendelea kumiminika kupata elimu kuhusu namna sahihi ya kuomba mkopo pamoja na huduma nyingine zinazotolewa na taasisi hizo.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mhe. Khadija Salum Ali, leo Julai 24, 2026, ametembelea banda la HESLB na kupokea maelezo kuhusu utoaji wa elimu ya mikopo ya wanafunzi pamoja na huduma shirikishi zinazotolewa, hususan kuwawezesha waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2026/2027 kuelewa sifa, vigezo na taratibu za kuomba mkopo kwa usahihi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Chakechake, Mhe. Zuhura Mgeni Othman, jana Julai 23, 2026, alitembelea banda la HESLB na kuipongeza bodi hiyo kwa kuhakikisha changamoto nyingi zinazohusiana na uombaji wa mikopo zinapatiwa ufumbuzi katika eneo moja, baada ya kujionea maafisa wa NIDA na NaPA wakiendelea kutoa huduma ndani ya banda la HESLB.
Maonesho hayo ya siku tano yenye kaulimbiu isemayo “Ubunifu na Taaluma ni Msingi wa Maendeleo” yalianza Julai 23 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 27, 2026, katika Uwanja wa Gombani, Pemba.
