Bi. Reshma Bharmal-Shariff, Ofisa Mtendaji Mkuu BrighterMonday Tanzania
KAMPUNI ya ajira ya BrighterMonday Tanzania imezindua mpango unaoitwa ‘Umoja Wakati wa Shida ‘ ambao utatoa nafasi kwa watu binafsi au kampuni kutangaza ajira bure katika kipindi hiki ambacho nchi inapambana na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kampuni hiyo jijini Dar es Salaam kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Reshma Bharmal-Shariff ilieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kuongeza juhudi za biashara nchini.
“Kampeni inalenga kuendeleza shughuli za biashara na ajira kwa kuwezesha mashirika kupata watu wenye uwezo wa utendaji hasa unaokidhi tija ya nyakati za sasa za changamoto.
“Katika kipindi cha miezi mitatu ijayo, tutawapa waajiri fursa ya kuajiri wataalamu katika tasnia tofauti kwa kuwawezesha waajiri kutangaza kazi kwenye tovuti yetu. Hii itawezesha hospitali, vituo vya huduma ya afya na watoa huduma wengine muhimu katika mapambano dhidi ya corona kuajiri wataalamu waliofuzu viwango, katika kipindi cha muda mfupi kadri itakavyowezekana,” alisema Reshma.
Alisema kupitia mpango huo, waajiri wataweza kufuatilia mchakato mzima wa kuajiri na kupata huduma zingine zilizobuniwa na BrighterMonday ikiwemo zana ya tathmini ya ustadi wa kampuni hiyo ambayo inapima uwezo wa msingi wa waombaji wa ajira na stadi za ziada zinazohitajika katika kazi husika zaidi ya ile iliyowekwa kwenye wasifu (CV) zao wakati wa mchakato wa kuajiri.
“Kwa kuongezea, waajiri wataweza kuona alama za mwombaji mbali na ujuzi mwingine uliozoeleka wa elimu na viwango vya uzoefu ikiwamo matumizi ya mfumo wa Ufuatiliaji wa Maombi wa BrighterMonday (ATS), ambao unarahisisha kufanya tathimini kwa mwombaji wa ajira husika.
“Hivyo kwa njia hii wataweza kulinganisha ustadi, sifa na viwango vya uzoefu wa mwombaji wa nafasi husika, BrighterMonday Tanzania tupo hapa kwa ajili yako jana, leo na hata kesho,” alisema Reshma.