Mkuu wa Wilaya ya Temeke (DC), Sixtus Mapunda, amesema njia madhubuti ya kumaliza biashara ya dawa za kulevya nchini ni kukata cheni ya biashara hiyo kwa kupunguza idadi ya watumiaji kupitia elimu na ushirikiano wa jamii, akisisitiza kuwa bila wateja biashara hiyo itakosa soko.
Mapunda amesema pamoja na juhudi zinazoendelea za kudhibiti uzalishaji, usafirishaji na uhifadhi wa dawa za kulevya, hatua hizo bado zinakabiliwa na changamoto kutokana na mbinu mbalimbali zinazotumiwa na wahalifu, hivyo jamii ina wajibu mkubwa wa kuzuia matumizi ya dawa hizo.
“Siku tusipokuwa na watumiaji, maana yake tumeshakata cheni. Kwenye biashara yoyote, demand ndiyo inaleta supply. Ukikata uhitaji, mzigo utakosa soko,” amesema.
Amesema wazazi wanapaswa kuanza kuwapa watoto elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya tangu wanapoanza kupata ufahamu ili kuwajengea uwezo wa kukataa vishawishi vinavyoweza kuharibu maisha yao.
Aidha, amewatahadharisha vijana kutojaribu kutumia dawa za kulevya kwa kudhani ni fasheni au starehe, akieleza kuwa athari zake huanza taratibu na kufikia hatua ambayo huwa vigumu kurekebisha.
Mapunda amesema alipotembelea banda la Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya aliona sampuli mbalimbali za dawa hizo, zikiwemo bidhaa zinazotumiwa na baadhi ya wanafunzi wa sekondari na vyuo vikuu katika sherehe binafsi, jambo alilosema ni tishio kwa mustakabali wa vijana na taifa kwa ujumla.
Pia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kufuatilia mitandao ya biashara ya dawa za kulevya pamoja na mifumo ya utakatishaji fedha, akieleza kuwa maisha ya anasa yasiyo na maelezo yanaweza kuwashawishi baadhi ya vijana kuingia katika biashara hiyo haramu.
Vilevile, amewataka wananchi kuacha kuwaficha wafanyabiashara wa dawa za kulevya na badala yake kutoa taarifa kwa mamlaka husika, akisisitiza kuwa dawa hizo hufika hadi kwenye mitaa kutokana na baadhi ya wananchi kufumbia macho vitendo hivyo.
Akihitimisha, DC Mapunda amesema mapambano dhidi ya dawa za kulevya yanahitaji ushirikiano wa serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, wazazi, viongozi wa jamii na wananchi wote ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya janga hilo.

