Na Mwandishi Wetu,Mbinga

TAASISI ya Kidoti Foundation chini ya Mkurugenzi wake Joketi Mwegelo kwa kushirikiana na Umoja Super Cup,imepanga kufanya maboresho makubwa ya uwanja wa mpira wa miguu wa Tazama uliopo kijiji cha Tanga Halmashauri ya Mji Mbinga.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Kidoti Foundation Diwani wa kata ya Utiri Herswid Komba alisema,hatua hiyo itasaidia kuibua vipaji kwa vijana wa kijiji hicho na wilaya ya Mbinga kwa ujumla waweze kuonyesha vipaji walivyonavyo na  kupata nafasi ya kusajiliwa kwenye timu kubwa ikiwemo Simba na Yanga.

Komba alisema hayo jana baada ya kumalizika mchezo wa fainali wa mashindano ya Kidoti Foundation na Umoja Super Cup katika kijiji cha Tanga uliozikutanisha timu ya Nyundo na Barcelona.

Amezipongeza Timu zote zilizoshiriki katika mashindano hayo na amehaidi kuendelea kufadhili michezo kwa kutoa zawadi mbalimbali, ili  wilaya ya Mbinga  ing’are kimichezo kama ilivyo wilaya nyingine hapa nchini.

“Kidoti Foundation hatuna bla bla,tumejipanga kuinua vijana,kuibua  fursa na vipaji kwa vijana na kuboresha sekta  nzima ya michezo katika wilaya yetu ya Mbinga,kama ilivyo sera ya nchi yetu”alisema Komba. 

Ameipongeza kamati ya maandalizi chini ya mratibu wake Deo Mbele,kwa kuratibu vizuri mashindano hayo yaliyowasaidia vijana kupata nafasi ya kushiriki michezo,kuonyesha vipaji vyao,kuepuka kufanya vitendo viovu ikiwemo anasa,wizi na  ukatili kwenye maeneo yao. 

Aidha Komba,amewataka vijana wilayani humo kuendelea kudumisha na kulinda amani kwa kuwa vijana ndiyo walinzi na nguzo ya nchi yetu.

Awali Mratibu wa mashindano hayo Deo Komba alisema mashindano hayo yaliendeshwa kwa mfumo wa ligi na jumla ya timu 14 kutoka kata ya Myangayanga,Luwahita,Mbinga mji na kata ya Mateka zilishiriki kwenye mashindano hayo.

Alisema,mashindano hayo yalianza kwenye makundi mawili yenye timu saba kila kundi na timu nane ziliingia kwenye robo fainali,timu nne ziliingia kwenye nusu fainali  kabla ya kupata timu mbili ambazo zilifanikiwa kuingia fainali.

Katika mchezo wa fainali Timu ya Nyundo kutoka kijiji cha Zomba imekabidiwa zawaidi ya Sh.500,000 baada ya kuwa mabingwa wa mashindano hayo kwa kuifunga Timu ya Barcelona ya kijiji cha Tanga magori 3-0 ambayo ilipata zawadi ya Sh.200,000 na mshindi wa tatu Timu ya Beila kutoka kata ya Mateka imepata Sh.100,000. 

Mlinda mlango  wa Timu ya Nyundo Heri Nyoni, amepata Sh.100,000 baada ya kuwa golikipa bora wa mashindano hayo.