Na. Fullshangwe Blog, Dodoma
Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Mhe. Gelasius Byakanwa, amesema kuwa amefurahishwa na mafanikio ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) katika kuwahudumia watoto kutoka Burundi waliofanyiwa upasuaji wa moyo, akieleza kuwa hospitali hiyo imeiheshimisha Tanzania na kuiweka katika kiwango kingine cha utoaji wa huduma za afya.
Ameyasema hayo Julai 17, 2026, alipotembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kuwaona watoto kutoka Burundi waliofanyiwa upasuaji wa moyo hospitalini hapo, ambapo aliambatana na Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Leontine Nzeyimana.
Amesema kuwa alipoanza kutafuta ufadhili wa watoto hao kuja kutibiwa nchini Tanzania alikuwa na hofu kwa kuwa hakuwahi kushuhudia upasuaji wa aina hiyo ukifanywa kwa wagonjwa kutoka nje ya nchi, lakini aliamua kuwaamini wataalamu wa BMH na kuwahamasisha wazazi wa watoto hao.
Ameongeza kuwa BMH imeilipa imani hiyo kwa kiwango kikubwa na kuwapongeza madaktari na watumishi wa hospitali hiyo kwa kazi waliyoifanya.
Aidha, amesema kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya kisasa na vifaa vya tiba pamoja na kuwekeza katika kuwajengea uwezo wataalamu wa afya, hali iliyoiwezesha BMH kutoa huduma za viwango vya kimataifa.
Balozi Byakanwa amebainisha kuwa kwa maendeleo aliyoyashuhudia anaamini ndani ya miaka 20 ijayo Hospitali ya Benjamin Mkapa inaweza kuwa kituo kikubwa cha huduma za matibabu kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Afrika na hata dunia.
Kwa upande wake, Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Mhe. Leontine Nzeyimana, amesema kuwa ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi unapaswa kuendelea kuimarishwa kupitia sekta mbalimbali ikiwemo afya ili wananchi wa nchi hizo mbili wanufaike na uhusiano huo.
Ameongeza kuwa ameendelea kujifunza kutoka kwa Balozi Gelasius Byakanwa kutokana na jitihada zake mbalimbali za kuhudumia wananchi na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi.
Kwa upande wake , Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa Balozi Byakanwa ameonesha uzalendo na ubinadamu kwa kuwasaidia watoto kutoka Burundi kupata huduma za matibabu nchini Tanzania.
Amesema kuwa kila binadamu ana haki ya kupata huduma za afya bila kujali anatoka nchi gani na kwamba jitihada za Balozi Byakanwa zimeiwezesha BMH kuwahudumia wananchi hao.
Prof. Makubi amebainisha kuwa mafanikio ya hospitali hiyo yamechangiwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia uboreshaji wa miundombinu, vifaa tiba, mafunzo na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya.
Pia amesema kuwa huduma za kibingwa na bingwa bobezi zinazotolewa BMH zimeendelea kutambulika kimataifa, huku wataalamu kutoka mataifa mbalimbali wakishuhudia uwezo wa hospitali hiyo pamoja na vifaa tiba vya kisasa vilivyopo.
( PICHA ZOTE NA FULLSHANGWE BLOG)
