■ Utekelezaji wake mbioni kukamilika
■ Wafanyabiashara wausubiri kwa hamu
Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO
Ule msemo wa Kiswahili unaosema “Mgeni njoo, mwenyeji apone” unaendelea kupata uhalisia kupitia ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato, mradi mkubwa unaotekelezwa na Serikali jijini Dodoma.
Mbali na kuimarisha usafiri wa anga nchini, mradi huo tayari umeanza kuleta manufaa kwa wananchi kupitia ajira, biashara na fursa za uwekezaji, huku ukitarajiwa kuifanya Dodoma kuwa kitovu muhimu cha uchumi na usafiri wa anga.
Mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 370 unatarajiwa kukamilika Septemba 2026. Kwa sasa, ujenzi wa miundombinu umefikia asilimia 87.97, huku ujenzi wa majengo ukiwa umefikia asilimia 76.15.
Ajira Zimefungua Milango ya Mafanikio
Tangu ulipoanza mwaka 2022, mamia ya wakazi wa Dodoma wamepata ajira za muda na fursa za biashara zilizoongeza kipato cha familia zao.
Mkazi wa Mpamaa, Maximilian Mwagike, ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo. Anasema alianza kuuza miwa kwa kutumia baiskeli, lakini kuongezeka kwa shughuli za ujenzi kulipanua soko lake kiasi cha sasa kutumia guta kusafirisha bidhaa zake.
*”Biashara hii imenibadilisha maisha. Nimeboresha makazi yangu, ninalipia watoto wangu ada za shule binafsi na nimepanua biashara yangu,”* anasema Mwagike, ambaye pia amepata ajira ya usimamizi wa mazingira katika mradi huo.
Kwa upande wake, Mama Juma, aliyekuwa mama wa nyumbani, anasema mradi ulimwezesha kuanzisha biashara ya kupika na kuuza chakula kwa wafanyakazi wa ujenzi.
*”Leo naweza kulipia watoto wangu ada za shule, nimeweza kununua pikipiki inayoniingizia kipato na nina uhakika wa kuendelea na biashara hata baada ya mradi kukamilika,”* anasema.
*Mradi Wajenga Ujuzi kwa Vijana*
Mbali na ajira za moja kwa moja, mradi huu umechangia kuwajengea vijana ujuzi na uzoefu wa kazi. Adam Kiula, anayefanya kazi katika kampuni inayosimika mifumo ya TEHAMA, kamera za usalama na mawasiliano, anasema amepata maarifa na uzoefu unaomuwezesha kushindana katika soko la ajira.
Anawahimiza vijana kutumia kikamilifu fursa zinazotokana na miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali badala ya kusubiri ajira za kawaida.
*Wafanyabiashara Wanatazamia Mapinduzi ya Uchumi*
Faida za uwanja huo zinatarajiwa kuonekana zaidi baada ya kuanza kutoa huduma. Mfanyabiashara wa vifaa vya simu jijini Dodoma, anayefahamika kwa jina la Jeshi, anasema uwanja huo utarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka nje ya nchi na kupunguza gharama zinazotokana na kupitisha bidhaa kupitia Dar es Salaam.
Naye mfanyabiashara wa bidhaa za urembo, Happiness Mgeani, anaamini kukamilika kwa uwanja huo kutapunguza hasara zinazotokana na ucheleweshaji na uhamishaji wa mizigo kutoka usafiri mmoja kwenda mwingine.
*Uwanja wa Hadhi ya Kimataifa*
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zuhura Amani, anasema kazi zilizobaki ziko katika hatua za mwisho za ukamilishaji, zikiwemo ufungaji wa mifumo mbalimbali, taa za kuongozea ndege, alama za barabara za ndege na umaliziaji wa majengo.
Anasema uwanja huo umejengwa kwa viwango vya kimataifa na utakuwa na uwezo wa kupokea ndege kubwa kama Airbus A330 na Boeing 787 Dreamliner, pamoja na kuhudumia (maegesho) ndege 17 kwa wakati mmoja.
Aidha, anaeleza kuwa uwanja huo utakuwa na mnara wa kisasa wa kuongozea ndege wenye urefu wa mita 56.2, mnara wa pili kwa urefu Afrika Mashariki, pamoja na maeneo ya biashara, maegesho ya magari na nafasi ya upanuzi wa baadaye.
*Maandalizi ya Uendeshaji Yamekamilika*
Kwa upande wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Zacharo Mduma amesema maandalizi ya kuanza uendeshaji wa uwanja huo yanaendelea, ikiwa ni pamoja na kuandaa watumishi watakaotoa huduma za uhamiaji, forodha, afya, usalama na zimamoto mara baada ya mradi kukabidhiwa rasmi.
*Lango Jipya la Ukuaji wa Uchumi*
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unatarajiwa kuwa wa Daraja F, kiwango cha juu kinachotambulika kimataifa. Mradi huo umefadhiliwa kwa asilimia 85 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), huku Serikali ya Tanzania ikichangia asilimia 15.
Baada ya kukamilika, uwanja huo unatarajiwa kuhudumia zaidi ya abiria milioni 1.5 kwa mwaka na kuwa lango jipya la biashara, utalii na uwekezaji. Zaidi ya miundombinu ya usafiri, Uwanja wa Ndege wa Msalato unatajwa kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa Dodoma na Taifa kwa ujumla, huku ukiendelea kuthibitisha kwamba miradi mikubwa ya maendeleo inaweza kubadili maisha ya wananchi hata kabla haijakamilika.

