NA DENIS MLOWE IRINGA
MWENYEKITI wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Aggrey Tonga, amesema vijana wa mkoa huo ni miongoni mwa wanufaika wakubwa wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiwataka wananchi kuendelea kuitunza na kuisimamia ili iendelee kuleta manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Aggrey alitoa kauli hiyo wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa iliyotembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Iringa.
Alisema kamati hiyo imeshuhudia utekelezaji wa miradi katika sekta za elimu, afya, barabara, pamoja na miradi ya umwagiliaji na kilimo ambayo imeendelea kuboresha maisha ya wananchi.
“Miradi yote tuliyoitembelea inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwaletea wananchi maendeleo vijana ndiyo wanufaika wakubwa wa miradi hii kupitia ajira, biashara na fursa mbalimbali za kiuchumi,” alisema Aggrey.
Akizungumzia mradi wa upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Iringa, alisema si mradi wa Mkoa wa Iringa pekee bali ni mradi wa kimkakati wa kitaifa unaochochea ukuaji wa uchumi na utalii.
Alisema uwanja huo umewezesha mashirika mbalimbali ya ndege kutoa huduma Iringa, hali iliyoongeza idadi ya wageni, watalii na wafanyabiashara wanaofika mkoani humo.
“Hoteli zimeanza kupata wateja wengi zaidi, watalii wanaokwenda Hifadhi ya Taifa ya Ruaha wameongezeka na vijana wengi wamepata ajira kupitia shughuli zinazohusiana na usafiri, utalii na huduma mbalimbali,” alisema.
Aliongeza kuwa uwanja huo umefungua masoko mapya kwa wakulima wa Iringa kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao kwenda maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi kwa haraka.
Tonga aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo inayowanufaisha vijana na kusisitiza umuhimu wa kuisimamia vizuri ili iendelee kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
Awali, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Hosea Machaka, akiwasilisha taarifa ya mradi huo alisema ujenzi wa jengo jipya la abiria ulianzishwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Uwanja wa Ndege wa Iringa.
Alisema mradi huo unatekelezwa na kampuni ya China Harbour Engineering Company (CHEC) kwa usimamizi wa TANROADS kwa kushirikiana na mshauri elekezi Howard Humphreys Consulting Limited, huku ukifadhiliwa na Benki ya Dunia.
Machaka alisema mradi huo unagharimu shilingi bilioni 41.066 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 18.
Alieleza kuwa kazi zinazotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la kisasa la abiria, eneo la utabiri wa hali ya hewa, barabara za ndani na barabara unganishi, maegesho ya magari, mifumo ya kisasa ya usalama, mitaro ya kupitisha maji pamoja na uwekaji wa taa na alama za usalama.
Kwa mujibu wa Machaka, utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri ambapo ujenzi wa kambi za mkandarasi na mshauri elekezi umekamilika kwa asilimia 100, kazi za uchimbaji na misingi zimekamilika, ujenzi wa nguzo umefikia asilimia 98, kazi za kumwaga zege zinaendelea na zimefikia asilimia 60 huku ufungaji wa mifumo ya huduma za mitambo ukiwa umefikia asilimia 20.
Aliongeza kuwa hadi sasa mkandarasi amelipwa zaidi ya shilingi bilioni 10.57 na kwamba mradi unaendelea bila changamoto yoyote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri nchini.
Alisema Serikali imeendelea kuboresha viwanja vya ndege katika maeneo mbalimbali nchini, huku Mkoa wa Iringa ukiwa miongoni mwa mikoa iliyonufaika na uwekezaji huo mkubwa unaotarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi, biashara na utalii.

