Serikali ya Tanzania imepokea vifaa vya kisasa vya Chumba cha Kanzi Data (Data Centre), vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na miundombinu iliyoboreshwa ya mtandao kutoka Mamlaka ya Taifa ya Nyaraka na Kumbukumbu ya Sultanate ya Oman, hatua inayotarajiwa kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali katika mfumo wa kidijitali.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Jakaya Kikwete, alisema msaada huo ni sehemu ya ushirikiano unaoendelea kati ya Tanzania na Oman katika kuimarisha utawala bora na matumizi ya teknolojia kwenye huduma za umma. 

Ridhiwani amesema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza usalama wa taarifa za Serikali, kuboresha upatikanaji wa nyaraka kwa wakati, kuimarisha uhifadhi wa muda mrefu wa kumbukumbu muhimu za taifa pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema hatua hiyo pia ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa uhusiano wa kihistoria na ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sultanate ya Oman katika sekta mbalimbali za maendeleo.

“Ushirikiano huu unaonesha dhamira ya pamoja ya kujenga mifumo ya kisasa ya usimamizi wa kumbukumbu na nyaraka kwa kutumia teknolojia za kidijitali, jambo litakaloongeza ufanisi na uwajibikaji katika utumishi wa umma,” 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi kutoka Serikali za Tanzania na Oman, akiwemo Balozi wa Sultanate ya Oman nchini Tanzania, Said Hilal Al-Shidhani, Balozi Abdallah Kilima kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pamoja na viongozi na watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka.