Na Mwandishi wetu, Mirerani
KAMPUNI ya Franone Mining & Gem LTD imenufaisha jamii mbalimbali Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kupitia miradi tofauti ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya elimu, afya na miundombinu, kupitia uwajibikaji kwa jamii (CSR).
Meneja wa kampuni ya Franone Mining & Gem LTD, Sweetbert Arbogast ameeleza hayo kwenye ziara ya ujumbe wa shirika la Miss World ulipotembelea eneo la madini ya Tanzanite kitalu C mji mdogo wa Mirerani.
Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Miss World, Julia Morley lenye makao makuu yake jijini London, Uingereza na mnyange Miss World Africa 2025 Hasset Dereje wa Ethiopia.
Arbogast ameeleza kuwa miradi hiyo iliyotekelezwa na Franone Mining kwa ajili ya kusaidia jamii imefanyika katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Simanjiro.
Ametaja baadhi ya mradi hiyo ni ujenzi wa zahanati kwenye migodi ya madini ya Tanzanite na ukarabati wa barabara ya kilomita nane inayopanda kwenye machimbo hayo.
“Pia Franone imetoa madawati 100 kwa shule ya sekondari Mirerani B.W.Mkapa, ujenzi wa miundombinu ya madarasa shule ya sekondari Naisinyai na ujenzi wa miundombinu ya kituo cha afya Mirerani,” amesema Arbogast.
Ameeleza kuwa kwenye kipindi cha mafuriko yaliyotokea mwaka 2024 walitoa msaada wa chakula kwenye Tarafa ya Moipo na Kata ya Msitu wa Tembo na wanafunzi wa shule ya msingi Oloshonyokie.
Ofisa madini mkazi Mirerani (RMO) George Kaseza amesema eneo tengefu la Mirerani kuna vitalu mbalimbali vinavyochimbwa madini ya vito ya Tanzanite.
Kaseza ameeleza kwamba sehemu hiyo ina maeneo tofauti ambapo kuna kitalu A, B, C na D ambapo wachimbaji wenye migodi wamepewa leseni za kuchimba madini ya Tanzanite.
Katibu wa chama cha wachimbaji madini mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani Rachel Njau amesema ugeni huo ni mzuri kwao kwani utatumika kutangazwa zaidi kwa madini hayo ya vito ya Tanzanite kimataifa.
Mwenyekiti wa wanawake wafanyabiashara wa magonga, Magreth Sogweda, amesema wamepata faraja kutembelewa na ugeni huo kwani wameongezewa nguvu na moyo zaidi wa kazi wanazozifanya zinazidi kuthaminiwa.
Mwenyekiti wa chama cha wafanyabiashara wa madini mkoa wa Manyara, (Magebomita) Mokia Ole Mrefu amesema ugeni huo ni wakimataifa hivyo ni fursa nzuri kwa madini ya Tanzanite kuzidi kutangazwa na kufahamika zaidi.
