Na Peter Haule na Joseph Mahumi, WF, Tanga
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), amesema Serikali itafuatilia kwa karibu changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara ya Pangani-Tanga ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma kwa wananchi pamoja na kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi.
Mhe. Balozi Omar alitoa kauli hiyo alipotembelea mradi wa ujenzi wa sehemu ya barabara ya Pangani mkoani Tanga yenye urefu wa kilometa 50 kwa kiwango cha lami, ambayo ni sehemu ya mradi mkubwa wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)–Saadani–Pangani yenye urefu wa kilometa 256.
Ziara hiyo inafuatia kilio cha uongozi wa mkoa na Wilaya ya Tanga pamoja na wakazi wa Wilaya ya Tanga wanaoathirika na ubovu wa barabara hiyo unaokwamisha shughuli zao za kiuchumi hususan wakati wa mvua na masika.
Alisema mradi huo umechelewa kukamilika kwa muda mrefu, hali inayolazimu Serikali kuangalia kwa kina changamoto zinazouchelewesha ili kuhakikisha unakamilika na wananchi wanaanza kunufaika na huduma za usafiri na usafirishaji.
“Mradi huu ni muhimu kwa maendeleo ya wananchi na uchumi wa nchi. Tutafuatilia changamoto zinazoukabili ili utekelezaji wake ukamilike kwa wakati na uweze kutoa huduma iliyokusudiwa,” alisema Mhe. Balozi Omar.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara nchini-TANROADS Mkoa wa Tanga, Bw. Jotrevas August, alisema kuwa Mkandarasi anasuasua kukamilisha mradi licha ya juhudi za Serikali kuwataka watekeleze ujenzi wa mradi huo kwa wakati.
Alisema kuwa mazungumzo yanaendelea kati ya Serikali na Mkandarasi huyo, ambaye ni Kampuni ya ujenzi ya CHICO kutoka China ili atafute rasilimali fedha kwa ajili ya kukamilisha mradi huo.
Alisema hadi sasa kazi mbalimbali zimeendelea vizuri, ikiwemo kusafisha eneo la barabara kwa urefu wa kilometa 44.45, sawa na asilimia 88.9 ya kazi hiyo.
Aidha, ujenzi wa madaraja pamoja na matengenezo ya barabara ya awali na ya mchepuko kwa kiwango cha changarawe unaendelea sambamba na hatua nyingine za utekelezaji wa mradi.
Bw. August alisema kuwa mradi huo utakuwa kiungo muhimu kinachounganisha Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mombasa, hatua itakayoongeza ufanisi wa biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mradi wa barabara ya Bagamoyo (Makurunge)-Saadani-Pangani unatarajiwa kuwa moja ya miundombinu muhimu ya kimkakati itakayorahisisha usafiri, kuimarisha biashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa pwani na nchi jirani za Afrika Mashariki.

