Mkuu wa Wilaya ya Moshi, *Mhe. Godfrey Mnzava*, amezindua rasmi mitambo miwili ya ukarabati wa barabara yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 600, iliyonunuliwa kwa ushirikiano wa Wabunge wa Jimbo la Moshi Vijijini, *Mhe. Morris Makoi*, pamoja na Mbunge wa Jimbo la Vunjo, *Mhe. Enock Koola*, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu ya barabara katika majimbo hayo mawili.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, *Mhe. Mnzava* alisema mitambo hiyo ni uwekezaji mkubwa unaolenga kuongeza kasi ya ukarabati wa barabara za vijijini, kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao, pamoja na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.

Alisisitiza kuwa mafanikio ya uwekezaji huo yatategemea namna wananchi watakavyoshiriki kuilinda na kuitunza mitambo hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.

“Mitambo hii Kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha inalindwa na kutunzwa ili iweze kutumika kwa ufanisi katika kuboresha barabara za kata na vijiji vyetu,” alisema Mhe. Mnzava.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya aliwapongeza wabunge wa Moshi Vijijini na Vunjo kwa kuendelea kutekeleza ahadi walizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni, akieleza kuwa hatua yao ya kununua mitambo hiyo inaonesha dhamira ya kweli ya kutatua changamoto za miundombinu na kuharakisha maendeleo. 

Alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais *Dkt. Samia Suluhu Hassan* imeendelea kuweka mazingira mazuri ya maendeleo, huku viongozi wa majimbo wakitakiwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika kutekeleza miradi yenye manufaa kwa jamii.

Kwa upande wao, *Mhe. Morris Makoi* na *Mhe. Enock Koola* walisema ununuzi wa mitambo hiyo umetokana na kilio cha muda mrefu cha wananchi kuhusu ubovu wa barabara katika maeneo mbalimbali ya Moshi Vijijini na Vunjo.

Wabunge hao walieleza kuwa mitambo hiyo itasaidia kufanya matengenezo ya mara kwa mara ya barabara, kufungua njia zinazopitika wakati wote wa mwaka, kupunguza gharama za ukarabati na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Wananchi waliohudhuria hafla hiyo walieleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema itarahisisha shughuli za kiuchumi, hususan usafirishaji wa mazao ya kilimo, upatikanaji wa huduma za afya na elimu, pamoja na kuchochea ukuaji wa uchumi katika kata na vijiji vya majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo.

Uzinduzi wa mitambo hiyo unaashiria hatua muhimu katika kuimarisha miundombinu ya barabara na kuendeleza juhudi za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia usimamizi madhubuti wa rasilimali na ushirikiano wa viongozi wa majimbo hayo mawili.