Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la taifa la uwezeshaji wananchi kiuchumi Gwakisa Bapala wakati akizungumza na washiriki wa mafunzo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika wilayani Nkasi.

Baadhi ya wananchi walioshiriki katika mafunzo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika wilayani Nkasi
Na Neema Mtuka, Nkasi
Rukwa: Wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa za mitaji, pamoja na kujifunza vigezo na taratibu za upatikanaji wake kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo, Julai 14, 2026, na Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Gwakisa Bapala, katika mafunzo ya utoaji wa elimu kuhusu fursa za mitaji kupitia mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi yaliyofanyika wilayani Nkasi, mkoani Rukwa.
Bapala amesema lengo la mafunzo hayo ni kuitambulisha mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ili kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa za mitaji zinazopatikana katika sekta mbalimbali nchini.
Aidha, amesema kuwa kuna mifuko zaidi ya 75 inayotoa mikopo ya moja kwa moja, ikiwemo mifuko 62 ya Serikali na 13 ya sekta binafsi.
“Katika mafunzo haya, wananchi wa Mkoa wa Rukwa watajifunza namna ya kunufaika na fursa za mitaji na kufahamu ruzuku zinazotolewa ili kuendeleza biashara zao kwa kutumia mifuko hiyo,” amesema Bapala.
“Tutaendelea kutoa elimu kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanaifahamu mifuko hii ambayo ni rafiki, sambamba na fursa za upatikanaji wa ajira,” ameongeza.
Ameeleza kuwa kila mwaka NEEC huandaa maonesho kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi, ambapo kwa mwaka huu maonesho hayo yanatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba jijini Mwanza.
Amesema mifuko hiyo inapatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii, viwanda, kilimo na sekta ya fedha, huku NEEC ikiendelea kutoa elimu kuhusu huduma za biashara na njia rahisi za urejeshaji wa mikopo.
Mafunzo hayo yalianza Julai 13 na yanatarajiwa kuhitimishwa Julai 16, 2026, yakihusisha wilaya zote za Mkoa wa Rukwa.
