KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Daudi Yassin, imetembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 23.6 katika Wilaya ya Mufindi, ikiwemo barabara ya kiwango cha lami ya Mtiri–Ifwagi pamoja na mtambo wa kuzalisha oksijeni tiba katika Hospitali ya Mji Mafinga.Mradi mkubwa wa barabara ya Mtiri–Ifwagi wenye urefu wa kilomita 14 umegharimu shilingi bilioni 21.9, huku mradi wa mtambo wa kuzalisha oksijeni tiba katika Hospitali ya Mji Mafinga ukigharimu shilingi bilioni 1.78, fedha zilizotolewa kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo.
Akiwasilisha taarifa ya mradi wa barabara, kwa. Kamati ya Siasa,Meneja wa Tarura Mkoa wa Iringa Injinia Davies Tembo alisema kuwa barabara hiyo ilijengwa chini ya Mradi wa RISE (Roads to Inclusion and Socioeconomic Opportunities), unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, kupitia Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Wizara ya Ujenzi.
Alisema kuwa mradi huo ulianza Julai 27, 2023 na kukamilika Desemba 28, 2024, huku kipindi cha uangalizi wa mkandarasi (Defects Liability Period) kikimalizika Juni 30 mwaka huu.
Injinia Tembo alisema kuwa ujenzi wa barabara umehusisha kukata milima, kupasua miamba, kujenga madaraja mawili, makalavati 37, kuweka tabaka mbalimbali za barabara pamoja na kufunga taa za barabarani 90.
Aidha, maeneo yenye miteremko mikali yalijengwa kwa zege ili kuongeza uimara wa miundombinu hiyo na kukamilika kwa barabara hiyo kumerahisisha usafirishaji wa mazao ya misitu, chai, mboga mboga na mazao mengine ya biashara, kupunguza gharama za usafiri, pamoja na kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya, elimu na huduma za kiutawala kwa wananchi wa Ifwagi na maeneo jirani.
Kamati hiyo pia ilikagua mradi wa mtambo wa kuzalisha oksijeni tiba katika Hospitali ya Mji Mafinga uliotekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1,781,750,519.23 kupitia fedha za Serikali Kuu na Global Fund.
Mganga Mkuu wa halmashauri ya Mji Mafinga Dkt Bonaventula Chitopela akieleelezea kuwa mtambo huo una uwezo wa kuzalisha mitungi 60 ya oksijeni yenye ujazo wa lita 100 kwa siku na umeongeza kwa kiwango kikubwa ubora wa huduma za afya kwa wagonjwa wa dharura, wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), watoto wachanga pamoja na wajawazito.
Aidha, ulieleza kuwa kabla ya uwepo wa mtambo huo hospitali ilikuwa ikitumia wastani wa shilingi milioni tisa kununua oksijeni, lakini gharama hizo zimepungua hadi kufikia milioni nne kwa mwezi, hali inayookoa takribani shilingi milioni tano kila mwezi.
Hospitali hiyo pia imekuwa ikisambaza oksijeni tiba katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Hospitali ya Manispaa ya Iringa, Hospitali ya Ipamba pamoja na vituo vingine vya kutolea huduma za afya.
Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yassin, alisema Kamati ya Siasa imeridhishwa na ubora wa utekelezaji wa miradi hiyo kwani imeleta matokeo chanya kwa wananchi.
Alisema mradi wa mtambo wa oksijeni umeondoa changamoto ya upatikanaji wa huduma za dharura na kupunguza gharama za matibabu, huku barabara ya Mtiri–Ifwagi ikiwa imefungua fursa mpya za kiuchumi kwa wakazi wa Mufindi.
Yassin aliwataka wananchi kuendelea kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Alisema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya CCM na kwamba wananchi wa Mufindi ni mashahidi wa ahadi zilizotekelezwa na serikali.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ifwagi, Arafat Benson Mwambule, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupeleka fedha za ujenzi wa barabara hiyo, akisema tayari imeanza kuleta mabadiliko makubwa ya maendeleo katika eneo hilo na kwamba wananchi wana matarajio makubwa ya kuendelea kwa ujenzi wa kilomita nyingine zilizopangwa.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ifwagi, Fransis Bilangulo, alisema barabara hiyo imebadilisha sura ya kijiji na kuongeza shughuli za maendeleo, akieleza kuwa wananchi wanaiona Ifwagi kuwa miongoni mwa maeneo yaliyonufaika zaidi na uwekezaji wa serikali katika miundombinu.
Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa ni sehemu ya ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na kutathmini maendeleo ya miradi inayotekelezwa na Serikali katika Wilaya ya Mufindi na itaendelea kesho kwa wilaya ya Iringa.

