Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imepata Tuzo ya Mshindi wa Pili wa Mtoa Huduma Bora katika kategoria ya Mamlaka za Udhibiti, kwenye hafla ya kufunga Maonesho ya Kimataifa ya Biashara, maarufu kama Sabasaba, iliyofanyika leo, Julai 13, 2026, jijini Dar es Salaam mbele ya Mgeni Rasmi, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Meneja wa PPRA Kanda ya Pwani, Bi. Vicky Mollel, aliwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha usimamizi bora wa sekta ya ununuzi wa umma nchini kupitia Mamlaka hiyo.
“Tuzo hii inatokana pia na huduma bora tuliyoitoa kwenye maonesho haya tangu Juni 28, 2026, kuhusu matumizi ya Mfumo wa NeST katika kupata zabuni za umma, pamoja na elimu kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma. Watumishi walifanya kazi kwa ari na ubunifu, na pia tulikuwa na mazingira bora katika mabanda yetu mawili,” alisema Bi. Mollel.
Aliongeza kuwa tuzo hiyo imekuja siku chache baada ya Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Bw. Dennis Simba, kupokea Tuzo ya Kimataifa jijini Geneva, Uswisi, kwa niaba ya Serikali, baada ya Mfumo wa NeST kutambuliwa kuwa miongoni mwa mifumo 20 bora zaidi duniani katika sekta ya Serikali Mtandao (e-Government).
Mshindi wa kwanza katika kategoria ya Mamlaka za Udhibiti kwenye Maonesho ya Sabasaba mwaka huu ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
