Na. Fullshangwe Blog
Katibu Mkuu wa wizara ya Elimu, sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo amesema kuwa ni wakati muafaka wa kutafakari upya namna elimu inavyotolewa pamoja na aina ya kozi zinazotolewa katika taasisi za elimu ili ziendane na mahitaji ya dunia ya sasa na soko la ajira.
Ameyasma hayo Julai 13, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha mwaka cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.
Amesema kuwa baada ya kutangazwa kwa matokeo ya Kidato cha Sita amekuwa akifuatilia mijadala mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kozi zinazopaswa kusomwa na wahitimu hao ili waweze kuajiriwa au kujiajiri.
Amebainisha kuwa mijadala hiyo inaonyesha kuwa Watanzania wana matarajio mapya kuhusu aina ya elimu na kozi zinazohitajika katika dunia ya sasa, huku baadhi ya kozi zinazoshauriwa kutosomwa zikiwa bado zinatolewa katika taasisi za elimu nchini.
Pia amesema kuwa maoni hayo kutoka kwa jamii yanapaswa kuwa mrejesho kwa wizara na taasisi zake ili kutafakari upya programu za masomo na kuongeza nyingine zitakazokidhi mahitaji ya sasa, sambamba na kuzifanya ziwe rahisi zaidi kwa wanafunzi kuzisoma.
Aidha, amebainisha kuwa baadhi ya vyuo vikuu na vyuo vya kati tayari vimeanza kuandaa programu mpya zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira na amevipongeza kwa hatua hiyo, huku akibainisha kuwa bado kuna haja ya kuongeza programu nyingine kulingana na mabadiliko ya dunia.
Huku akibainisha kuwa wizara ina jukumu la kufanya skills mapping ili kubaini mahitaji ya ujuzi nchini na kuwaandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji hayo kwa kushirikiana na sekta mbalimbali.
Aidha, amesema kuwa kupitia miradi mbalimbali, taasisi za elimu zimeanza kujenga mifumo ya kushirikiana na waajiri pamoja na viwanda ili kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji halisi ya soko la ajira.
Aidha, amebainisha kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ndiyo msingi na mwelekeo wa utendaji kazi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Amesema kila shughuli na mpango utakaotekelezwa na wizara hiyo utalenga kufanikisha malengo yaliyobainishwa katika Dira hiyo.
Pia, amebainisha kuwa Wizara ya Elimu ina jukumu kubwa katika utekelezaji wa Dira ya 2050, hususan katika kuandaa rasilimali watu yenye ujuzi na uwezo unaohitajika. Ameeleza kuwa utekelezaji wa Dira hiyo utategemea ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, ambapo Serikali itachangia asilimia 30 na sekta binafsi asilimia 70.
Pia amebainisha kuwa mkakati wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) tayari umeandaliwa, huku akibainisha kuwa haupaswi kubaki kwenye makaratasi bali utekelezwe kwa vitendo.
Ameongeza kuwa kila taasisi inapaswa kutafuta mbinu zinazofaa za kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya sekta ya elimu.

