Katibu wa Chama cha Mapinduzi(CCM)Mkoa wa Ruvuma Mohamed Khalifan kushoto na Mwekezaji Omari Msigwa (Superfeo) wakitiliana saini makubaliano ya ujenzi wa mradi wa fremu za biashara katika eneo la Soko kuu Manispaa ya Songea lililogharimu zaidi ya Sh.milioni 500.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Mohamed Khalfan kushoto na Mwekezaji Mkurugenzi wa Kampuni ya Superfeo&Selou Expres Omari Msigwa kulia,wakibadilishana hati za ujenzi wa jengo la ghorofa moja ambalo litatumika kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo lililojengwa katika eneo la Soko kuu Manispaa ya Songea.

Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Mohamed Khalfan kushoto na Mwekezaji Mkurugenzi wa Kampuni ya Superfeo&Selou Expres Omari Msigwa kulia,wakionyesha hati za makubaliano ya ujenzi wa mradi wa jengo la biashara lililojengwa katika eneo la Soko kuu Manispaa ya Songea.

Katibu wa CCM Mkoa wa Ruvuma Mohamed Khalfan,akizungumza baada ya kutiliana saini makubaliano ya ujenzi wa Jengo la Biashara kati ya Chama cha Mapinduzi na mfanyabiashara maarufu wa Mkoa huo Omari Msigwa(Super Feo)jengo lililogharimu zaidi ya Sh.milioni 560,katikati mfanyabiashara huyo na kulia Mwenyekiti wa CCM Oddo Mwisho.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho,akizungumza na wanachama na baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Songea,wakati wa kutiliana saini makubailiano ya ujenzi wa jengo la Biashara eneo la Soko kuu la Manispaa ya Songea kati ya Chama hicho na Mwekezaji Omari Msigwa(Super Feo).
……….
Na Mwandishi Wetu, Songea
CHAMA cha Mapinduzi Mkoani Ruvuma kimesema,kitaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wazawa kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Kauli hiyo imetolewa jana Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma Oddo Mwisho,wakati wa hafla ya kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa fremu za maduka kati ya CCM na mwekezaji Omari Msigwa(Super Feo) mradi unaojengwa kwa gharama ya Sh.milioni 500.
Alisema, kupitia mradi huo CCM inalenga sio tu kujenga jengo la kisasa,bali kuchochea ukuaji wa mji wa Songea,kuongeza ajira pamoja na kutoa fursa mpya kwa wafanyabiashara wadogo na wakati.
“Mradi huu unaakisi dira na malengo ya Chama cha Mapinduzi ya kuendeleza miradi mbalimbali Mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanapata maeneo ya kisasa ya kibiashara yenye mvuto na tija kiuchumi”alisema
Mwisho alieleza kuwa, mradi huo wa ghoroa moja ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi wa Chama na kuongeza vyanzo vya mapato vitakavyosaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo kwa manufaa ya wananchi.
Alisema,ujenzi wa ghorofa hilo unaonesha dhamira ya CCM ya kuendelea kuwekeza katika miradi yenye tija, kujenga misingi imara ya kujitegemea kiuchumi, na kuifanya Ruvuma kuendelea kuwa kitovu cha maendeleo na fursa za uwekezaji.
“Tunampongeza mwekezaji Ndugu Omary Msigwa (Super Feo) kwa ushirikiano wake na Chama Cha Mapinduzi katika kufanikisha mradi huu muhimu, Tunatarajia kuona utekelezaji wa mradi huu ukikamilika kwa wakati na kwa viwango bora ili uwe chachu ya maendeleo ya Mkoa wa Ruvuma”alisema.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma Mohamed Khalfan alisema,mradi wa fremu za biashara utaleta manufaa makubwa kwa Chama na Mkoa wa Ruvuma,utapanua vyanzo vya mapato,utatoa mazingira bora ya biashara kwa wafanyabiashara na kuongeza thamani ya eneo hilo muhimu kibiashara katika Manispaa ya Songea.
Aidha alisema, katika kipindi cha miaka mitatu CCM Mkoa wa Ruvuma imeanzisha na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo ni ujenzi wa kupaki magari,karakana na kituo cha mauzo ya mkaa wa mawe wa majumbani katika eneo la Seedfarm wenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 560.
“Mradi huu tayari umeanza kukipatia Chama mapato takribani Sh.milioni 42 kwa mwaka,huu ni uthibitisho kuwa uwekezaji huu unaleta matokeo chanya na unaendelea kuimarisha uwezo wetu kujitegemea kifedha”alisema Khalfan.
Pia alisema, Chama kimejenga fremu 25 eneo la Majimaji pamoja na vibanda vya Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) vilivyojengwa kwa gharama ya Sh.milioni 42 na miradi hiyo imeongeza thamani ya mali za Chama,imezalisha fursa za biashara kwa wananchi na kuongeza mapato ya kudumu ya Chama.
Kwa upande wake Mwekezaji Omari Msigwa alisema,ujenzi wa mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na jengo hilo litadumu kwa muda wa zaidi ya miaka mia moja na amekishukuru Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Ruvuma kwa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi.
Alisema,eneo hilo ni muhimu hasa kwa ajili ya uwekezaji kwani hapo awali kulikuwa na makontena na Chama hakikupata mapato makubwa,lakini kupitia ujenzi huo sasa Chama kitapata mapato stahiki.
Naye Afisa miradi wa Chama hicho Tommy Mwaifunga alisema,CCM Mkoa wa Ruvuma ina miradi sita inayomilikiwa na kusimamiwa na Chama hicho na ipo katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea ambayo kwa sasa inaingiza mapato Sh.milioni 32,050,000 kwa mwezi.
Alisema kuwa miradi hiyo inajumuisha nyumba 71 za makazi,fremu 90 za biashara,uwanja wa mpira wa miguu wa Majimaji,Hoteli maarufu ya Majimaji,ukumbi wa Jambolee na maeneo ya wazi na mradi unaingiza kiasi cha Sh.milioni 14,530,000 kwa mwezi.
Alisema, jengo hilo litakuwa na fremu 50 za biashara na litagharimu kiasi cha Sh.milioni 300 katika awamu ya kwanza na tayari fremu 25 zimekamilika.
Mwaifunga alisema,katika utekelezaji wa mradi huo fremu 27 chakavu zilizokuwa zinaingiza Sh.1,900,000 kwa mwezi zimeondolewa na chini ya mkataba wa miaka mitano unaomalizika mwaka 2030 CCM Mkoa wa Ruvuma inaingiza Sh.3,840,000.
Alisema,asilimia 40 ya mapato yanayotokana na kodi na asilimia 60 ikitumika kurejesha gharama za uwekezaji na baada ya mkataba kukamilika mapato yanatarajiwa kufikia Sh.9,900,000 kwa mwezi.
