Na Silivia Amandius 

Bukoba.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Kanali Yahya Ramadhani Kido, amewataka watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji, uadilifu na weledi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, akisisitiza kuwa wao ni wawakilishi wa Rais katika kuwahudumia wananchi.

Mhe. Kido ametoa maelekezo hayo leo, Julai 11, 2026, alipokutana na viongozi pamoja na watumishi wa umma katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba (Chemba).

Amesema mafanikio ya utumishi wa umma yanategemea mshikamano, ushirikiano na kuepuka migogoro mahali pa kazi, hali ambayo huchochea utoaji wa huduma kwa ufanisi na kuongeza imani ya wananchi kwa Serikali.

Aidha, amewasisitiza watumishi kusikiliza na kushughulikia kwa wakati kero za wananchi pamoja na kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili ilete matokeo yaliyokusudiwa.

Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa amewahimiza kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kwa kuepuka vitendo vinavyoweza kuichafua Serikali na badala yake kuilinda, kuitetea na kutekeleza sera na miongozo yake kwa uaminifu.

Kwa niaba ya watumishi, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Bi. Felister Shayo, ameahidi kuwa watumishi wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, ufanisi na kuzingatia malengo ya Serikali katika kuwahudumia wananchi.