Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu Mbadala na Elimu ya Watu Wazima Zanzibar, Bi. Mashavu Ahmda Fakhi, ameipongeza Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza sekta ya elimu nchini, akisema imeendelea kuwa mdau muhimu wa kuhakikisha Watanzania wa Bara na Zanzibar wanapata elimu bora kupitia uboreshaji wa miundombinu na uwekezaji katika maendeleo ya elimu.
Bi. Mashavu aliyasema hayo Julai 11, 2026, alipotembelea banda la TEA katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo alisema TEA imekuwa mstari wa mbele kusimamia utekelezaji wa miradi ya elimu inayowezesha mageuzi ya sekta hiyo kwenda sambamba na mtaala mpya unaolenga kuwajengea wanafunzi ujuzi na umahiri unaohitajika katika soko la ajira na maendeleo ya taifa.
“Ninaishukuru sana TEA kwa kazi kubwa mnayoifanya. Ni wadau wakuu wa maendeleo ya elimu Tanzania Bara na Zanzibar. Mmeendelea kuhakikisha miundombinu ya elimu inaimarika na wanafunzi wanapata elimu bora yenye ujuzi na umahiri, kwa sababu elimu ndiyo ufunguo wa maisha na msingi wa maendeleo ya uchumi wa taifa,” alisema Bi. Mashavu.
Aidha, aliwataka wadau wa maendeleo ya sekta ya elimu, ndani na nje ya nchi, kuendelea kuunga mkono juhudi za TEA kwa kuchangia Mfuko wa Elimu wa Taifa ili kuongeza uwezo wa mamlaka hiyo kufadhili miradi ya elimu nchini.
“Natoa rai kwa wadau wote wa maendeleo ya sekta ya elimu waweze kuchangia Mfuko wa TEA. Kadiri mfuko unavyokuwa na rasilimali za kutosha, ndivyo mamlaka itakavyoweza kufanya makubwa zaidi katika kuboresha elimu. Lengo letu ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata elimu bora yenye tija kwa maendeleo yake binafsi na kwa uchumi wa taifa,” alisisitiza.

