Na Mwandishi Wetu
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, ametembelea banda la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), ambapo amepongeza juhudi zinazofanywa na mamlaka hiyo katika kudhibiti bidhaa duni na bandia za afya kwa lengo la kulinda afya ya wananchi.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Dkt. Magembe alisema TMDA inaendelea kutekeleza jukumu muhimu la kuhakikisha bidhaa za afya zinazotumika nchini zinakidhi viwango vya ubora, usalama na ufanisi, huku akiitaka mamlaka hiyo kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya bidhaa za afya.
Alisisitiza kuwa TMDA inapaswa kutumia watoa huduma za afya ngazi ya jamii kufikisha elimu kwa wananchi ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya dawa na bidhaa nyingine za afya, hatua ambayo itasaidia kupunguza madhara yanayotokana na matumizi yasiyo sahihi ya bidhaa hizo.
“Tumieni watoa huduma wa ngazi ya jamii kusaidia kufikisha elimu kuhusu matumizi salama ya bidhaa za afya ili kulinda wananchi. TMDA mnafanya kazi nzuri na hongereni sana,” alisema Dkt. Magembe.
TMDA inashiriki katika Maonesho ya Sabasaba kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kutambua bidhaa duni na bandia za afya, matumizi sahihi ya dawa pamoja na majukumu yake ya udhibiti wa dawa, vifaa tiba na bidhaa nyingine za afya. Maonesho hayo yanaendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam, hadi Julai 13, 2026.
