Na Jeremia Mwakyoma na Jeremiah Mbwambo
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA – JULAI 10, 2026
Kliniki ya Wateja Maalumu, wa Kimataifa na uchunguzi wa Afya wa Kina (Royal, International Patients and Master Health Check up Clinic) katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) leo imetimiza mwaka mmoja kwa mafanikio tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati wa Hafla ya kutimiza mwaka mmoja, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amesema kuwa hiyo ni clinic ya kwanza inayotoa huduma za uchunguzi wa Kibingwa wa Afya na kutoa matibabu kwa haraka ndani ya muda mfupi na kumpa mgonjwa mazingira mazuri kati yake na wataalamu wanaomuhudumia.
“Wateja wazawa na wanaotoka nje ya nchi wanapata huduma za kibobezi kwenye clinic hii, ndani ya dakika 15 wanakuwa wameshaonana na Mabingwa Bobezi, huduma zote muhimu zinatolewa hapa ndani ya klinic hii ikiwemo za maabara na vipimo, Famasi na huduma za malipo ndani ya muda mfupi ili kumuondolea mteja usumbufu” amesisitiza Prof. Makubi
Kiongozi wa Kliniki hiyo Dkt. Saguda Nilla amesema huduma zinawavutia wazawa na wageni kutoka nje ya Tanzania, kwa mwaka huo wa kwanza wamehudumia zaidi ya Wateja 28,000 huku zaidi ya 200 wakitoka nje ya Tanzania na wengine zaidi ya 300 wamefanya uchunguzi wa Afya wa kina bila kuwa wanaumwa na kujua.hali za Afya zao.
Nao Wateja wameendelea kupongeza huduma za kliniki hiyo, Bi. Sara Lenday kutoka Iringa amesema kuwa huduma ni za haraka, alitoka Iringa akamleta mama yake kupata matibabu ya moyo wakafanikiwa na kurudi Iringa siku hiyohoyo.
Nae Deogratias Haule amesema kuwa yeye hajiskii kuumwa ila amekwenda Kliniki ya Royal kupata huduma za uchunguzi wa Afya wa Kina na huwa anafanya uchunguzi huo kila mwaka na kutoa wito kwa Watanzania kuwa na utamaduni wa kuchunguza Afya kila mwaka ili kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.

