Na Fullshangwe Blog, Dodoma
Watoto watatu kati ya Sita wenye matatizo ya matundu ya moyo kutoka nchini Burundi wamefanyiwa upasuaji kuziba matundu ya moyo Kwa mafanikio katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kupitia ushirikiano kati ya BMH, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na wataalamu wa afya kutoka Burundi, hatua inayoweka msingi wa ushirikiano wa kikanda katika utoaji wa huduma za kibingwa na kukuza tiba utalii nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari Julai 9, 2026 jijini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof. Abel Makubi, amesema kuwa watoto wote waliopatiwa matibabu wanaendelea vizuri na wameonyesha maendeleo ya kuridhisha baada ya kufanyiwa upasuaji huo.
Prof. Makubi amesema mafanikio hayo yanaonyesha uwezo wa taasisi za afya nchini kushirikiana katika kutoa huduma za kibingwa zinazokidhi viwango vya kimataifa, huku akibainisha kuwa ushirikiano huo umefungua fursa ya kubadilishana ujuzi na uzoefu kati ya wataalamu wa Tanzania na Burundi.
Aidha, Amebainisha kuwa mafanikio hayo yametokana na uwekezaji uliofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuboresha miundombinu, vifaa tiba na kuendeleza rasilimali watu, hatua iliyowezesha hospitali za umma kutoa huduma ambazo hapo awali zilihitaji wagonjwa kwenda nje ya nchi.
Pia, amebainisha Kuwa sekta ya afya imeendelea kuimarishwa kwa kuweka mazingira yanayowawezesha wataalamu kufanya kazi kwa weledi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, Dkt. Godwin Godfrey amesema ushirikiano huo umeongeza uzoefu na mbinu mpya kwa wataalamu wa Tanzania katika matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto.
Amesema kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma za kibingwa, ni muhimu taasisi za afya kuendelea kushirikiana ili kuongeza ufanisi wa huduma na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
Kwa upande wake, mmoja wa wazazi wa watoto waliopatiwa huduma hiyo, Shedrack Nizigyimana, ameishukuru Serikali, BMH, JKCI na madaktari wote waliohusika kwa kufanikisha upasuaji huo, akisema awali familia yake iliamini huduma za aina hiyo zinapatikana nje ya nchi pekee.
“Sasa tuna imani kubwa na hospitali zetu. Watoto wetu wamepata huduma bora na tunaona maendeleo yao. Tutaendelea kuitangaza Tanzania kwa mafanikio haya makubwa katika huduma za afya,” amesema.
Naye daktari kutoka Burundi, Dkt. Nzitunga Aimie Jeanne Carmen Octavie, amesema ushirikiano kati ya wataalamu wa Tanzania na Burundi umewezesha kubadilishana uzoefu na kuimarisha uwezo wa timu za matibabu.
Imeelezwa kuwa watoto hao walizaliwa na kasoro za kimaumbile katika muundo wa moyo zilizohitaji matibabu ya kibingwa ili kurejesha utendaji sahihi wa moyo.

