Na. Calvin Katera – Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji (Mb) ametoa maagizo sita kwa Kamishna wa Uhifadhi TANAPA Massana Mwishawa leo Julai 09, 2026, jijini Arusha alipokuwa akiongoza zoezi la uapisho kwa aliyekuwa Naibu Kamishna wa Uhifadhi baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan Julai 02, 2026 kuchukua nafasi ya Kamishna wa Uhifadhi (Mstaafu) CPA Musa Nassoro Kuji aliyemaliza muda wake.

Akizungumza katika hafla ya uapisho huo Waziri Kijaji amemwelekeza Kamishna Mwishawa kusimamia miundombinu ya hifadhi, kuvutia wawekezaji, kubuni bidhaa mpya za utalii, kusimamia mapato, kuimarisha uhusiano na jamii zinazozunguka maeneo ya hifadhi bila kusahau nidhamu, uadilifu, weledi, ustawi wa watumishi na kusimamia maslahi yao kwa wakati.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Mkuu wa Majeshi (Mst.) Jenerali George Waitara alieleza kuwa Bodi itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati na ushauri wakati wote ili kufanikisha adhma ya kuendeleza sekta ya maliasili na utalii.

Pia alisisitiza kuwa uendeshaji wa shughuli za Shirika zifanywe kwa uwazi na utoaji wa mrejesho uwahusishe maafisa na askari ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Uhifadhi Massana Gibril Mwishawa alibainisha kuwa Hifadhi za Taifa ni hazina kubwa ya kiikolojia, kiuchumi, na kijamii na zinachangia kwa kiasi kikubwa katika mapato ya serikali na miradi ya kimkakati kama uzalishaji wa umeme.

Akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana hiyo, Kamishna Mwishawa aliahidi kutekeleza majukumu yake kwa uzalendo, uadilifu, uwajibikaji, nidhamu, na weledi akishirikiana na watumishi wenzake.

Hafla hii imehudhuriwa na wakuu wa taasisi za uhifadhi ikiwemo NCAA, TFS na wawakilishi kutoka TAWA, viongozi wa Serikali, wadau wa uhifadhi na utalii, viongozi wa dini, Maafisa na Askari wa TANAPA.