Mstahiki Meya wa Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula amepongeza ushiriki wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba, 2026 akieleza kuwa maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kulitangaza jiji na fursa zake kwa wananchi na wawekezaji.

Alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwenye maonesho hayo yanayoendelea jijini Dar es Salaam, ambapo alipata nafasi ya kuelezwa huduma zinazotolewa, maeneo ya uwekezaji pamoja na fursa mbalimbali zinazopatikana ndani ya Jiji la Dodoma.

Chaula alisema kuwa ameridhishwa na ushiriki wa jiji katika maonesho hayo na kusisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu nafasi hiyo kujitangaza ili wananchi wanaotembelea banda hilo waweze kufahamu na kuvutiwa na fursa zilizopo ndani ya Jiji la Dodoma.

“Ni vizuri mkatumia maonesho haya kujitangaza kikamilifu, kueleza kwa uwazi huduma mnazotoa, maeneo ya uwekezaji na fursa mbalimbali zilizopo ndani ya jiji letu ili wananchi na wadau wanaotembelea banda hili waone umuhimu wa kuchangamkia fursa hizo” alisema Chaula.

Aidha, alisisitiza kuwa ushiriki wa Jiji la Dodoma katika Maonesho ya Sabasaba unapaswa kuwa chachu ya kuhamasisha uwekezaji, kukuza biashara na kutangaza vivutio pamoja na huduma zinazotolewa na halmashauri kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi ya jiji hilo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Jiji la Dodoma, Dennis Gondwe alisema kuwa ushiriki wa jiji katika maonesho hayo unalenga kuitangaza Dodoma kama makao makuu ya nchi, kuonesha fursa za uwekezaji zilizopo, huduma za ardhi, biashara pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na halmashauri kwa manufaa ya wananchi na wawekezaji.

Maonesho ya 50 ya biashara ya Kimataifa Sabasaba, 2026 yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi za umma na binafsi kuwasilisha huduma, bidhaa na fursa mbalimbali kwa wananchi huku yakitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu na kuongeza uelewa kuhusu masuala ya maendeleo na uchumi.