Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe ametoa maelekezo kwa Serikali ya Kijiji cha Mitondi A kilichopo kata ya Kitama kuhakikisha wanapanda miti mingine ya Mikorosho baada ya awali iliyokuwepo kukatwa.
Gavana Shilatu aliyasema hayo Leo Jumanne Aprili 7, 2020 wakati akizungumza na Halmashauri ya Serikali ya Kijiji cha Mitondi A ambapo alionyesha kuchukizwa na kitendo cha uamuzi wa kukata Mikorosho wakati hiyo ni sehemu ya uchumi na uhifadhi wa mazingira unaopazwa sauti kila kukicha na Serikali.
“Makosa mmekwisha fanya ya kukata Mikorosho, sasa mna jukumu la nyie mliosimamia ukatwaji huu kuhakikisha mnarudishia miti iliyokatwa. Hapa ni kata mti, panda mti tuendelee kuimarisha uchumi na mazingira” alisema Gavana Shilatu.
Gavana Shilatu alikemea vikali yeyote atakayeendelea ukataji Mikorosho na malumbano juu ya hili kwani atakuwa anachochea uvunjifu wa amani nae hayupo tayari kuona amani inatoweka.
“Yeyote atakayeendeleza zoezi la ukataji Mikorosho ama malumbano juu ya suala hili, Serikali tutamchukulia hatua kali kwani zoezi hili linaonekana kuwagawa Wananchi na hii ni hatari kiusalama. Tii sheria bila shurti.” Alisisitiza Gavana Shilatu
Katika kikao hicho ambacho Gavana Shilatu alialikwa kushiriki kilihudhuliwa pia na Diwani kata ya Kitama na Mtendaji kata ya Kitama.