Na Mwandishi Wetu, Mbinga
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas,ameipongeza Halmashauri ya Wilaya Mbinga kwa kupata hati safi kwa muda wa miaka kumi mfululilo huku Halmashauri hiyo ikifanikiwa kukusanya Sh.bilioni 13.4 kati ya lengo la kukusanya Sh.bilioni 10 hadi kufikia tarehe 30 Juni 2026.
Abbas, ametoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na watumishi na madiwani kwenye kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG) na maagizo ya Kamati ya kudumu la Bunge hesabu za Serikali za mitaa(LAAC)
“Mmeongeza Sh bilioni 3.4 hivyo mnastahili pongezi kubwa,nammshukuru Mheshimiwa Mbunge na Madiwani kwa namna mnavyoratibu vizuri Baraza linalopelekea kuwa na utulivu ukiacha changamoto chache ”alisema Rc Abbas.
Aidha,amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Joseph Kashushura na menejimenti yake kuweka mpango bora wa matumizi ya ardhi,hata hivyo amewataka waendelee kusimamia vizuri ili ardhi iliyopo iweze kuwanufaisha wananchi kwa muda mrefu.
“Ardhi hii haiongezeki ila matumizi yake ndiyo yanaongezeka,tujitahidi sana kutambua na kulinda ardhi kwa manufaa ya sasa na baadaye na kutatua migogoro ili kuwaondolea wananchi migogoro inayosababishwa na matumizi ya ardhi”alisema Rc Abbas.
Pia,mewataka watumishi wa afya kuepuka kuwatoza wananchi gharama ambazo hazistahili wanapofika kwenye vituo vya kutolea huduma za matibabu ikiwemo huduma za uzazi kwa akina mama.
Katika hatua nyingine Abbas, amezikumbusha Halmashauri zote nane za Mkoa huo, kuhakikisha mikopo ya asilimia kumi inayotolewa kwa makundi maalum ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu inakwenda kwa walengwa na wataalamu wawasaidie wananchi kujaza kwa usahihi maombi ili waweze kufikia vigezo vya kupata mikopo hiyo.
Katibu Tawala wa Mkoa huo Mary Makondo,ameitaka menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya Mbinga kuongeza bidii ili kufuta hoja zilizosalia kwa kuzifanyia kazi na kuweka suala la hoja kuwa ni agenda ya kudumu kwani muda uliobaki sio rafiki.
Makondo, ameipongeza menejimenti ya Halmashuri hiyo kwa hiyo na kuwataka kuendelea kuweka hesabu vizuri zitakazowezesha kuendelea kupata hati safi.
“Hati safi ni cheti cha uthibitisho kinachotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),kuwa taarifa za fedha za taasisi, Halmashauri zimeandaliwa kwa usahihi na fedha za umma zimetumika kwa uwazi, kufuata sheria, na taratibu zilizowekwa”alisema Makondo.
Makondo, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuupatia Mkoa wa Ruvuma fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwawezesha wananchi kuendelea kupata huduma bora za kijamii.
“Katika mwaka wa fedha 2026/2027 tumepitishiwa(kuhidhinishiwa) takribani bilioni 371 zinazojumuisha mishahara ya watumishi,stahili zao,uendeshaji wa ofisi pamoja na miradi ya maendeleo,tumekuwa tukipewa kipaumbele mwaka 2025/2026 tulipata Sh.bilioni 351”alisema Makondo.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioisha tarehe 30 Juni 2025 Mweka hazina wa Halmashauri hiyo CPA Samwel Marwa alisema,kulikuwa na hoja 22 za miaka ya nyuma ambapo hoja 12 zimefanyiwa kazi na hoja 10 zilizoabaki zinafanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa Marwa,mwaka 2024/2025 kulikuwa na hoja 28 ambapo hoja 9 zimefanyiwa kazi na hoja 19 bado zinaendelea kufanyiwa kazi na katika maagizo 4 ya kamati ya kudumu ya Bunge(LAAC)kulikuwa na hoja 4 kati ya hizo moja imefanyiwa kazi na 3 zinafanyiwa kazi.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa nje(CAG)Mkoa wa Ruvuma Nicholous Kilinga alisema,walifanya ukaguzi kwenye kitabu kikuu,mfuko wa wanawake,vijana na watu wenye ulemavu na mfuko wa pamoja wa afya na katika ukaguzi huo Halmashauri ya wilaya ya Mbinga imepata hati safi na haikuwa na dosari kubwa za taarifa za fedha.
Alisema,katika mwaka 2024/2025 Halmashauri hiyo ilikuwa na hoja 22 za miaka ya nyuma na imefunga hoja 11 sawa na asilimia 50 na kubakiwa na hoja 11.
Ameipongeza menejimenti ya Halmashauri kumtumia vizuri mkaguzi wa hesabu za ndani ambaye anafanya ukaguzi wa hesabu kwa kila robo mwaka na kuziwakilisha ofisi za CAG na amekuwa mstari wa mbele wa kufunga hoja kwa wakati.
