Na Farida Mangube Morogoro
Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) kwa kuzindua mashine za utoaji wa zana (kondomu) pamoja na huduma ya upimaji wa VVU kwa siri katika maeneo ya vyuo vikuu, ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kinga kwa wananchi, hususan vijana.
Akizungumza wakati wa ziara yake mkoani Morogoro, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Prof. Palamagamba Kabudi, amesema matumizi ya mashine hizo yataongeza upatikanaji wa zana za kinga na kuhamasisha wananchi kupima afya zao kwa hiari na kwa siri, hatua itakayochangia kupunguza maambukizi mapya ya VVU.
Prof. Kabudi amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa uwazi kuhusu matumizi ya mashine hizo ili kuondoa dhana potofu na kuhakikisha wananchi wanaelewa faida zake katika kujikinga dhidi ya maambukizi ya VVU na magonjwa mengine ya zinaa.
Amesema Serikali imeamua kununua na kusambaza mashine hizo kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha huduma za kinga na kuhakikisha zinapatikana kwa urahisi katika maeneo yenye makundi yaliyo katika hatari zaidi ya maambukizi.
Aidha, Prof. Kabudi amesema Serikali inalenga ifikapo mwaka 2030 kuwa na uwezo wa kuzalisha dawa mbalimbali nchini, zikiwemo dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV), ili kuongeza upatikanaji wake na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.
Kutokana na azma hiyo, amehimiza Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kuendelea kufanya tafiti kuhusu mimea tiba na kushirikiana na wadau wa sekta ya afya katika utafiti na ubunifu utakaowezesha uzalishaji wa dawa mbalimbali, ikiwemo ARV, kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini.
Awali, Prof. Kabudi aliwasili Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro ambako alisaini kitabu cha wageni na kupokea taarifa kuhusu ziara yake kabla ya kutembelea Kituo cha Afya cha Kingolwila kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Akiwa katika kituo hicho, Prof. Kabudi alimshauri Mkurugenzi wa Manispaa ya Morogoro kutafuta njia ya kupanua eneo la kituo hicho kwa kuwalipa fidia wananchi wa maeneo ya jirani ili kupata eneo la ziada au kujenga majengo ya ghorofa, akieleza kuwa kituo hicho kimebanwa na ukuaji wa mji unahitaji miundombinu ya afya inayoweza kukidhi mahitaji ya huduma kwa siku zijazo.

