Mkurugenzi wa Tanzania International Tourism Festival Ibrahim Jamal akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo.
Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA),Rukia Walele akizungumza kuhusu tamasha hilo jijini Arusha 
Mmoja wa wasanii  Simon Venance akionyesha bidhaa zake ambazo amekuwa akitengeneza.
…………
Na Happy Lazaro, Arusha
SEKTA ya utalii na sanaa nchini inatarajiwa kunufaika zaidi kupitia Tamasha la Sanaa na kazi za ufundi litakalofanyika Oktoba mwaka huu likiwa na lengo la kukuza sanaa za ufundi, kutangaza utamaduni wa Tanzania na kuwafungulia wasanii masoko ya ndani na nje ya nchi.
Tamasha hilo linaandaliwa na Tanzania International Tourism Festival (TITF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TASFA)ambapo  tamasha hilo litawakutanisha wachongaji, wachoraji na wabunifu wa kazi mbalimbali za mikono kutoka maeneo tofauti ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya GrandMelia Arusha,Mkurugenzi wa Tanzania International Tourism Festival ,Ibrahim Jamal amesema kuwa ,mbali na maonesho ya sanaa, washiriki watapata mafunzo kuhusu uongezaji thamani wa bidhaa zao, ulinzi wa kazi za ubunifu pamoja na mbinu za kufikia masoko ya ndani na kimataifa kupitia sekta ya utalii.
Ibrahimu amesema kuwa,tamasha hilo  linawakutanisha wasanii, wabunifu na mafundi wa kazi za mikono ili kuonyesha na kuuza bidhaa zao, kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya na kukuza uchumi wa ubunifu. Katika tamasha hilo hupatikana kazi mbalimbali kama uchoraji, uchongaji, ususi, ushonaji wa vitambaa, ufinyanzi, utengenezaji wa vito, bidhaa za ngozi, vikapu, mapambo ya asili na kazi nyingine za ubunifu.
“Mbali na maonesho ya sanaa na bidhaa za mikono, tamasha hilo huwa na mafunzo, warsha, maonesho ya moja kwa moja ya utengenezaji wa kazi za sanaa, burudani za muziki na ngoma za asili pamoja na fursa za wafanyabiashara na wanunuzi kukutana huku lengo lake ni kuhifadhi na kutangaza utamaduni, kuhamasisha utalii, kuwajengea uwezo wasanii na kuongeza fursa za ajira na kipato kupitia sekta ya sanaa na ubunifu. “amesema Ibrahim.
Ibrahim amesema kuwa ,washiriki watapatiwa mafunzo kuhusu mwenendo wa soko la sanaa ndani na nje ya Tanzania, thamani ya kazi zao, pamoja na nafasi ya sanaa katika kukuza utalii, utamaduni na kuongeza kipato cha wasanii na Taifa kwa ujumla.
Waandaaji pia wameandaa safari maalumu za kutembelea vivutio vya utalii vya mkoa wa Arusha, ambapo wageni na washiriki wa tamasha watapata fursa ya kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine muhimu ya utalii ili kujionea vivutio vinavyoitangaza Tanzania duniani.
Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA),Rukia Walele amesema kuwa , tamasha hilo ni hatua muhimu ya kuitangaza sekta ya sanaa za ufundi ambayo imekuwa ikitoa ajira kwa maelfu ya Watanzania lakini bado haijapata nafasi kubwa ya kutambulika.
Shirikisho hilo linasimamia fani mbalimbali za ubunifu zikiwemo uchongaji, uchoraji, ufinyanzi, ususi, ubunifu wa mavazi, utengenezaji wa bidhaa za ngozi na kazi nyingine za mikono zinazochangia maendeleo ya uchumi wa ubunifu nchini.
Naye Joseph Rumanyika kutoka TITF amesema kuwa,Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, likiwakutanisha wadau wa sanaa, utalii na utamaduni kutoka ndani na nje ya Tanzania, huku waandaaji wakiamini litakuwa chachu ya kuongeza thamani ya kazi za wasanii na kuitangaza Tanzania kupitia sanaa na utamaduni wake.
Naye Mmoja wa wasanii  akizungumzia tamasha hilo Simon Venance  amesema kuwa ,wanashukuru kwa fursa hiyo kwani umekuwa na mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali kwa wasanii, jambo ambalo limetupa uzoefu na maarifa ya kuboresha kazi zetu. 
“Ingawa bado kuna changamoto ya kupata fursa nyingi zaidi za mafunzo na matukio yanayowahusisha wasanii, kwa ujumla tunafurahia kuona vijana wakishirikiana na kufanya kazi kwa pamoja ili kukuza sekta ya sanaa.”amesema.
“Kama mchoraji, nimejipanga kwa kuandaa kazi zenye ubora wa hali ya juu ambazo ziwakilisha vipaji vyangu. Pia nimejikita katika kuandaa kazi zinazotangaza Tanzania kupitia utamaduni, historia na maisha ya watu wetu.”amesema
Amesema kuwa ,tamasha hili litawakutanisha watu kutoka ndani na nje ya Tanzania, hivyo ni fursa nzuri ya kuwaonesha wageni utamaduni wetu kupitia sanaa. 
“Mbali na kuitangaza Tanzania, pia litatusaidia kupata masoko mapya ya kazi zetu, kufanya biashara na kuuza bidhaa za sanaa.”amesema
Aidha amesema kuwa,wageni watapata nafasi ya kujifunza na kufahamu tamaduni za Tanzania kupitia kazi zetu za sanaa, jambo ambalo litachangia kuitangaza nchi yetu kimataifa.