Na Mwamvua Mwinyi-Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amezindua rasmi Mashindano ya 65 ya Riadha Kitaifa yanayofanyika katika Viwanja vya Filbert Bayi, Manispaa ya Kibaha, huku akisisitiza dhamira ya serikali ya mkoa kuifanya Pwani kuwa kitovu cha michezo nchini, sambamba na mafanikio yaliyopatikana katika uwekezaji, viwanda na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amewataka wanariadha kushindana kwa bidii, nidhamu na uzalendo, akieleza kuwa riadha ni miongoni mwa michezo iliyoitangaza Tanzania kimataifa kwa miaka mingi.
Amesema michezo ni chachu ya afya, ajira na ukuaji wa uchumi, hivyo Mkoa wa Pwani umejipanga kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo ili kuzalisha vipaji na kuongeza ushindani wa kitaifa na kimataifa.
Baada ya uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa alishuhudia mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanaume, ambapo mwanariadha Steward Mboya kutoka Mkoa wa Mbeya alijinyakulia medali ya dhahabu.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Shirikisho la Riadha Tanzania, Alfred Shahanga, alisema mashindano hayo yanalenga kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya wanariadha nchini.
Ameomba wadau mbalimbali waendelee kushirikiana na shirikisho hilo katika kukabiliana na changamoto za rasilimali fedha na upatikanaji wa vifaa vya michezo.
Mashindano hayo ya 65 ya Riadha Kitaifa yamewakutanisha wanariadha kutoka mikoa mbalimbali nchini chini ya kaulimbiu “Michezo Huleta Umoja, Amani na Mshikamano kwa Maendeleo ya Taifa,” yakilenga kuimarisha ushindani, kuibua vipaji na kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia mchezo wa riadha.


