NA FAUZIA MUSSA
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Hamida Mussa Khamis, amewataka wananchi na watumiaji wote wa barabara kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani ili kupunguza ajali zinazosababisha vifo, majeruhi na hasara zisizo za lazima.
Ameutoa wito huo wakati wa hafla ya kukabidhi mabango ya usalama barabarani kwa mabalozi wa usalama barabarani, yaliyotolewa na Taasisi ya Majlis Almaarif Islamia, hafla iliyofanyika katika Ofisini kwake Tunguu.
Hamida alisema usalama barabarani ni jukumu la kila mwananchi, hivyo kila mtu anapaswa kujilinda yeye mwenyewe na pia kuwalinda watumiaji wengine wa barabara, hususan makundi maalumu yakiwemo watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
“Wapo wanaoweza kujilinda wenyewe, lakini wapo wanaohitaji kulindwa. Hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake anapokuwa barabarani,” alisema.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali wanaojitolea kuimarisha usalama wa wananchi na kuahidi kuwa itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unaleta matokeo chanya.
” hatua iliyochukuliwa na majlis almaarif ni ya kupongezwa yenye kuonyesha dhamira yao ya dhati katika kusaidia usalama wa wengine hasa makundi maalum barabarani.”
Alifafanua kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa maendeleo katika mapambano dhidi ya ajali za barabarani, ambazo zimeendelea kuwa tishio kwa usalama wa wananchi na maendeleo ya jamii.
Alieleza kuwa Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya barabara kwa gharama kubwa, hivyo ni muhimu miundombinu hiyo itumike kwa usahihi na iwe chachu ya maendeleo badala ya kuwa chanzo cha ajali.
Aidha, alisema bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara kwa kuwa baadhi ya wananchi na madereva hawazingatii alama za usalama.
“Si kila raia anafahamu kuwa sehemu ya zebra ndiyo eneo salama la kuvuka barabara, na pia si kila dereva anaheshimu alama hizo. Hii inaonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa jamii,” alisisitiza.
Pamoja na hayo aliwataka mabalozi wa usalama barabarani kutumia vifaa walivyokabidhiwa kwa weledi na kuendelea kutoa taarifa za madereva wanaokiuka sheria za barabarani, ikiwemo wanaofanya misafara holela ya vyombo vya maringi mawili.
“Tunafahamu kazi mnayoifanya ni ya kujitolea na ya wito. Endeleeni kuitumikia jamii kwa moyo wa kujitolea mkitarajia malipo kutoka kwa Mwenyezi Mungu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Majlis Almaarif Islamia, Sheikh Tahir Khatib Tahir, alisema lengo la kugawa mabango hayo ni kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Alisema kuongezeka kwa miundombinu ya barabara ya lami katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar kumeongeza idadi ya vyombo vya usafiri na matumizi ya barabara, hali ambayo pia inachangia kuongezeka kwa ajali endapo tahadhari haitachukuliwa.
“Tumeshuhudia utekelezaji mkubwa wa miradi ya barabara kuu na za ndani, jambo lililosababisha kuongezeka kwa vyombo vya usafiri na matumizi ya barabara. Hivyo, mabango haya yatasaidia kuimarisha usalama wa wananchi,” alisema.
Sheikh Tahir alisema katika awamu ya kwanza ya mradi huo, mabango 350 yatasambazwa kwa mabalozi wa usalama barabarani katika mikoa yote ya Unguja, huku awamu inayofuata ikitarajiwa kuhamia katika mikoa ya Pemba.
Aidha, alibainisha kuwa taasisi hiyo ina mpango wa kuanzisha mfumo wa kidijitali wa kufuatilia wanaovunja sheria za usalama barabarani ambapo mabalozi watapatiwa simu janja zitakazounganishwa na mfumo huo ili kurahisisha utoaji wa taarifa za matukio ya ukiukwaji wa sheria.
Pamoja na hayo, alisema taasisi hiyo pia imejipanga kutoa mafunzo kwa mabalozi wa usalama barabarani ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Abdalla Salim Abdalla, anayejitolea kuvusha wanafunzi barabarani, alieleza masikitiko yake kutokana na baadhi ya madereva, hususan wa vyombo vya magurudumu mawili, kuwadharau na kuwakejeli mabalozi wanapotekeleza majukumu yao.
Kwa upande wake, balozi wa usalama barabarani kutoka Mwembeladu, Nassor Abeid Issa, aliiomba Serikali kuendelea kuwapa ushirikiano wanaporipoti matukio ya ukiukwaji wa sheria za barabarani.
Alishukuru majlis almaarif kwa msaada huo na kusema mabango hayo mapya ni makubwa na yanaonekana kwa urahisi zaidi, jambo litakalosaidia madereva wengi kuyazingatia na kutii sheria za usalama barabarani.
Akizungumza kwa niaba ya wadhamini wa mradi huo ofisa elimu kutoka mamlaka ya mapato zanzibar ( ZRA) Abdul- shakur Ramadhan alisema wataendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazolenga kusaidia kutatua changamoto za jamii ikiwemo usalama barabarani.

