Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe,Amesema elimu ni msingi wa maendeleo ya taifa, hivyo ni muhimu miundombinu inayojengwa itunzwe kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. 

Ameyasema hayo Julai 2, 2026, wakati wa uzinduzi wa kitaifa wa awamu ya pili ya Barrick-Twiga Future Forward Education Program uliofanyika Kibaigwa, mkoani Dodoma

Aidha, amebainisha Kuwa  Serikali inatambua mchango mkubwa wa Kampuni ya Barrick kupitia ubia wake na Serikali wa Twiga Minerals katika kuboresha sekta ya elimu kwa kuwekeza kwenye miundombinu inayowawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira bora.

Pia, ameishukuru Barrick kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu na kueleza kuwa ana imani ushirikiano huo utaendelea hata baada ya kukamilika kwa awamu ya pili ya mradi huo. Pia amesema mazungumzo ya ushirikiano huo yalifunguliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na sasa jukumu lililobaki ni kuendeleza mafanikio hayo.

Awali, Mkurugenzi Mkazi wa Barrick nchini, Dkt. Melkiory Ngido, alisema kampuni hiyo imeendelea kutekeleza ahadi yake ya kushirikiana na Serikali kuboresha elimu baada ya makubaliano ya mwaka 2023 ya kutoa zaidi ya shilingi bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, mabweni na matundu ya vyoo katika shule za sekondari nchini.

Amesema Kuwa kupitia awamu ya pili ya programu hiyo, Barrick imejenga madarasa sita pamoja na mabweni mawili yenye madawati na vitanda kwa wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaigwa.

Aidha, Dkt. Ngido, amebainisha Kuwa mradi huo unalenga kujenga madarasa 1,090, majengo ya vyoo 1,640 pamoja na mabweni 270 katika shule 161 nchini, hatua itakayowanufaisha takribani wanafunzi 190,000 wa kidato cha tano na sita.

Naye Meneja wa Fedha wa Barrick, Penina Kituku, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanapata elimu katika mazingira bora kupitia uwekezaji unaoboresha miundombinu ya elimu nchini.