WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekuwa ikifuatilia utendaji kazi wa watendaji wake ili kuhakikisha kuwa hakuna uzembe wa aina yoyote unatokea na kusababisha kuharibika kwa uchaguzi.
Amesema Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, zikisomwa pamoja na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na Sheria ya Ushahidi na kwa kuzingatia Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma, ikithibitika kuwa mtumishi husika ameharibu uchaguzi na kuisababishia Serikali hasara, atachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuachishwa kazi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 6, 2019) Bungeni jijini Dodoma kwenye mkutano wa 19 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema utaratibu upo wazi wa kushughulikia watendaji wa uchaguzi wanaofanya uzembe wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kwani NEC hutekeleza majukumu yake kwa uhuru na bila kufuata maagizo ya mtu yeyote.
“…kwa mujibu wa Ibara ya 74(7) na (11) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekuwa ikifanya kazi zake kwa weledi na kwa kuzingatia maelekezo ya Katiba, Sheria, Kanuni, Miongozo na Taratibu zilizopo.”
Waziri Mkuu ameongeza kuwa NEC imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali wa uchaguzi, mfano, kabla ya kuanza uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ilikutana na wadau wa uchaguzi katika ngazi ya Taifa na ngazi ya mikoa.
Amesema wadau hao ni pamoja na viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, wawakilishi wa Asasi za Kiraia, viongozi wa makundi maalum ya watu wenye ulemavu, vijana, wanawake, wahariri na waandishi wa habari.
Waziri Mkuu amesema lengo la ushirikishaji huo ni kuwataarifu kuhusu matakwa ya kisheria ya kuboresha Daftari, kupata maoni yao na kuwajengea wadau uelewa wa pamoja kuhusu uboreshaji.
Amesema kupitia mikutano, wadau wote waliafiki kuhusu taratibu zilizowekwa na Tume katika kutekeleza jukumu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Pia, Waziri Mkuu amesema vyama vya siasa vilielezwa haki ya kisheria ya kuweka mawakala katika vituo vya uboreshaji wa Daftari na wakati wote wa uboreshaji mawakala wa vyama mbalimbali walikuwemo vituoni.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema mwaka 2019/2020, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ilichunguza na kuvitaka baadhi ya Vyama vya Siasa vilivyotuhumiwa kuvunja katiba ya Nchi na Sheria ya Vyama vya Siasa kuwasilisha maelezo kwa Msajili. “Vyama hivyo, baada ya kutoa maelezo kwa Msajili, baadhi yake vilipewa adhabu mbalimbali ikiwemo onyo.”
Amesema katika kuhakikisha kuwa Vyama vya Siasa vinakidhi na kutekeleza matakwa ya Sheria zinazosimamiwa na Ofisi ya Msajilli wa Vyama vya Siasa, Ofisi inaendelea kuvifanyia uhakiki vyama vyote kuhusu utekelezaji wa masharti ya usajili na matakwa mengine ya Sheria ya Vyama vya Siasa na Sheria ya Gharama za Uchaguzi.