NA DENIS MLOWE
SERIKALI imeendelea kuvuna matunda ya uwekezaji katika sekta ya kilimo na miundombinu wilayani Iringa baada ya ongezeko la uzalishaji wa mpunga, kuimarika kwa viwanda vya kuchakata mazao na kufunguka kwa fursa mpya za ajira na biashara katika Tarafa ya Pawaga.
Mbunge wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtatifikolo Kaganda, alipotembelea Kiwanda cha Ndete Starch Q kilichopo katika Kijiji cha Itunundu, Kata ya Itunundu, kinachojihusisha na uchakataji wa mpunga kwa kutumia teknolojia ya kisasa.
Mtatifikolo alisema uwekezaji uliofanywa na Serikali katika maghala ya kuhifadhi mazao, umeme vijijini na skimu ya umwagiliaji ya Mkombozi umebadili kwa kiasi kikubwa maisha ya wakulima ambao sasa wana uwezo wa kuhifadhi mazao yao, kuyaongezea thamani na kuyauza kwa bei nzuri badala ya kuuza mpunga ghafi kwa walanguzi mara baada ya mavuno.
Alisema hapo awali wakulima wengi walikosa maeneo salama ya kuhifadhi mazao, hali iliyowalazimu kuuza mpunga kwa haraka kutokana na uhaba wa maghala na hofu ya kuibiwa, lakini sasa hali hiyo imebadilika kufuatia ujenzi wa maghala kupitia mpango wa Big Results Now.
Mbunge huyo alisema uwekezaji huo umeibua mnyororo mpana wa thamani ambapo pamoja na wakulima kunufaika, vijana wengi wamepata ajira kupitia shughuli za uchakataji, upakiaji na usafirishaji wa mchele.
Alisema Tarafa ya Pawaga kwa sasa ina viwanda 17 vya kuchakata mpunga, jambo linaloonyesha namna mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali yalivyowavutia wawekezaji binafsi.
“Serikali imefanikiwa kupeleka umeme vijijini na hilo limekuwa msingi mkubwa wa kuibuka kwa viwanda hivi. Kilichobaki sasa ni kuendelea kuboresha barabara ili kurahisisha usafirishaji wa mazao na kuongeza ushindani wa bidhaa zetu,” alisema.
Mtatifikolo alisema Serikali tayari imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 20 za barabara ya Pawaga kuelekea Iringa Mjini, huku zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zikitengwa kwa ajili ya kuendelea kujenga barabara ya Pawaga–Izazi na shilingi milioni 800 zikitengwa katika bajeti ya mwaka huu kuendeleza mradi huo.
Aidha alisema uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 56 katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mkombozi umeongeza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mpunga na mazao mengine ya biashara, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi wa wananchi na kuunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ndete Starch Q, Luka Ndete, alisema Pawaga imekuwa kitovu muhimu cha uzalishaji wa mpunga kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika umwagiliaji, nishati na miundombinu ya barabara.
Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika umewezesha viwanda kufanya kazi kwa ufanisi, huku ujenzi wa barabara ya kuelekea Izazi ukitarajiwa kurahisisha usafirishaji wa mchele kwenda masoko makubwa, hususan Mkoa wa Dodoma.
Ndete alisema maendeleo hayo yamechochea pia kilimo cha mazao mengine ya biashara kama vitunguu, nyanya na mboga mbalimbali, ambapo wakulima wengi sasa wanalima mashamba makubwa ya kibiashara tofauti na zamani walipolima kwa ajili ya kujikimu pekee.
Aliongeza kuwa ongezeko la shughuli za uzalishaji limefungua fursa kwa sekta nyingine ikiwemo usafirishaji, biashara za pembejeo, malazi na huduma mbalimbali zinazochangia kukuza uchumi wa eneo hilo.
Naye Afisa Tarafa wa Pawaga, Emanuel Ngabuji, alisema tarafa hiyo imeendelea kuwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa uzalishaji wa mpunga kutokana na uwekezaji mkubwa wa Serikali katika kilimo cha umwagiliaji.
Alisema kupitia Skimu ya Mkombozi pamoja na kuongezeka kwa viwanda vya kuchakata mpunga, wakulima sasa wanauza mchele ulioongezwa thamani badala ya kuuza mpunga ghafi, jambo linaloongeza kipato chao na kuifanya Pawaga kuwa kitovu muhimu cha biashara ya nafaka ndani na nje ya nchi.
Ngabuji alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha miundombinu ya umeme, barabara, maji na masoko ili kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuvutia uwekezaji zaidi katika Tarafa ya Pawaga na Wilaya ya Iringa kwa ujumla.

