Dar es Salaam, 27 Juni 2026 – Wafanyakazi wa Standard Chartered Bank Tanzania kwa kushirikiana na Nipe Fagio wameadhimisha miaka 20 ya mpango wa kujitolea kwa jamii wa Standard Chartered duniani kwa kufanya zoezi la usafi wa mazingira katika Ufukwe wa Silversand, Kunduchi jijini Dar es Salaam.

Zoezi hilo lililofanyika kama sehemu ya shughuli za kila mwaka za kujitolea kwa jamii, liliwaleta pamoja washiriki 74 wakiwemo watoto 20, kwa lengo la kuchangia uhifadhi wa mazingira ya pwani na kuhamasisha jamii kushiriki katika kulinda mazingira.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mtendaji Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Coverage wa Standard Chartered Bank Tanzania, Geofrey Mchangila, alisema maadhimisho hayo yana umuhimu mkubwa kwa kuwa yanaendana na kutimiza miaka 20 ya mpango wa kujitolea kwa jamii wa benki hiyo duniani kote.

“Zoezi la mwaka huu lina umuhimu wa pekee kwetu kwani linafanyika wakati Standard Chartered inaadhimisha miaka 20 ya kujitolea kwa jamii duniani kote. Tunaamini kuwa mabadiliko ya kweli huanza pale watu wanapounganisha nguvu zao,” alisema Mchangila.

Alisema kupitia ushirikiano wa wafanyakazi, familia zao pamoja na Nipe Fagio, benki hiyo itaendelea kuchangia katika kulinda ukanda wa pwani wa Tanzania na kujenga jamii zenye afya bora pamoja na mazingira endelevu kwa vizazi vijavyo.

Katika zoezi hilo, washiriki walifanikiwa kusafisha eneo lenye ukubwa wa takribani mita za mraba 4,000 za ufukwe na kukusanya kilo 506 za taka zilizowekwa kwenye mifuko 55.

Uchambuzi wa taka zilizokusanywa ulionesha kuwa taka za plastiki, hususan povu la polystyrene na chupa za plastiki za vinywaji, ndizo zilizokuwa nyingi zaidi, jambo linaloonesha umuhimu wa kuendelea kuchukua hatua madhubuti za kupunguza uchafuzi wa mazingira ya bahari.

Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, kupitia ushirikiano wake na Nipe Fagio, Standard Chartered Tanzania imeendesha jumla ya kampeni tano za usafi wa fukwe ambazo zimehusisha washiriki 594.

Kupitia kampeni hizo, benki hiyo imefanikiwa kusafisha zaidi ya mita za mraba 32,000 za ukanda wa pwani na kukusanya karibu tani tano za taka.

Mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Standard Chartered wa kuendeleza uhimilivu wa mazingira na maendeleo endelevu, sambamba na kuunga mkono Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), hususan Lengo la 13 linalohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, Lengo la 14 la kuhifadhi maisha ya chini ya maji na Lengo la 17 la kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya kufanikisha malengo.

Standard Chartered imeeleza kuwa itaendelea kuwahamasisha wafanyakazi wake kutumia muda, ujuzi na utaalamu wao katika kuleta mabadiliko chanya na endelevu katika jamii na mazingira kupitia programu mbalimbali za kujitolea.