Tanzania imezindua mfumo wa kidijitali wa Tanzania Chamber Portal (TCP) unaolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma za biashara, kupunguza changamoto za taratibu za kibiashara na kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara nchini.

Uzinduzi wa mfumo huo umefanyika Juni 30, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Majadiliano ya Biashara na Uwekezaji 2026, ukiwakutanisha viongozi wa Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo kwa ajili ya kujadili mageuzi ya biashara kupitia matumizi ya teknolojia.

Mfumo huo unaosimamiwa na Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TNCC) umeandaliwa kuwa sehemu moja ya kidijitali inayowawezesha wafanyabiashara kupata huduma mbalimbali ikiwemo kupata vyeti vya asili ya bidhaa (Certificates of Origin), kuripoti vikwazo visivyo vya ushuru na kupata taarifa muhimu za biashara.

Kupitia mfumo huo, Serikali inalenga kupunguza matumizi ya karatasi, kuongeza uwazi, kupunguza muda wa upatikanaji wa huduma na kushusha gharama za kufanya biashara, hususan kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto katika kupata huduma na taarifa za biashara.

Moja ya maboresho makubwa katika mfumo huo ni kuunganishwa kwake na Mfumo wa Dirisha Moja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA Single Window System), hatua itakayowezesha ubadilishanaji wa taarifa na nyaraka za biashara kwa njia ya kielektroniki kati ya taasisi mbalimbali za Serikali.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema mabadiliko ya uchumi wa Tanzania yanategemea ushirikiano mkubwa kati ya Serikali na sekta binafsi.

“Mustakabali wa uchumi wa Tanzania uko mikononi mwetu, lakini zaidi ya yote unategemea nguvu, ubunifu na ujasiri wa sekta binafsi. Hakuna nchi iliyofikia mabadiliko makubwa ya kiuchumi bila kuwa na sekta binafsi imara na yenye ushindani inayoungwa mkono na Serikali,” amesema.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema uzinduzi wa mfumo huo unaonesha hatua ya kutoka kwenye mipango ya kisera kwenda kwenye utoaji wa huduma halisi kwa wafanyabiashara.

“Mfumo huu siyo tu chombo cha kidijitali, bali ni sehemu ya juhudi pana za kufanya huduma za biashara zipatikane kwa urahisi zaidi, ziwe na ufanisi na ziendane na mahitaji ya wafanyabiashara kote nchini,” amesema.

Mfumo wa Tanzania Chamber Portal umeandaliwa kupitia mradi wa Tanzania Gateway for Trade, Transport and Environment (T-GATE) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia mpango wa Global Gateway Initiative, ukiwa na lengo la kuboresha biashara, usafirishaji na mazingira ya uwekezaji nchini.

Rais wa TNCC, Vicent Bruno Minja, amesema mfumo huo ni sehemu ya mageuzi ya Chama hicho katika kuboresha utoaji wa huduma na kuimarisha nafasi ya sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

“Kwa kuleta huduma muhimu mtandaoni, tunarahisisha wafanyabiashara na wawekezaji kupata msaada, kutatua changamoto na kushiriki kwa ufanisi zaidi katika uchumi wa Tanzania,” amesema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Nchi wa TradeMark Africa Tanzania, Solomon Michael, amesema mifumo ya kidijitali inapaswa kuleta matokeo yanayoonekana kwa wafanyabiashara kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma, utatuzi wa changamoto na kuongeza uhakika katika kufanya biashara.

Uzinduzi wa mfumo huo unaelezwa kuwa sehemu ya juhudi pana za Tanzania za kuunganisha mifumo ya forodha, utoaji wa vyeti, leseni na huduma za biashara ili kupunguza urudiaji wa taratibu, kushusha gharama za miamala na kuongeza ushindani wa Tanzania katika biashara ya kikanda na kimataifa.