Msajili wa Hazina, Bw. Nehemiah Mchechu akizungumza kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye hafla ya kupokea Gawio na Michango kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 30 Juni, 2026.

…………
Na. John Bukuku – Dar Es Salaam
Ofisi ya Msajili wa Hazina imeikabidhi Serikali gawio na michango mingine yenye thamani ya Sh1.32 trilioni zilizokusanywa hadi Juni 29, 2026 kutoka taasisi za umma pamoja na kampuni ambazo Serikali ina umiliki wa hisa.
Akizungumza Juni 30, 2026 katika hafla ya Siku ya Gawio iliyohudhuriwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mgeni rasmi, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema kuwa kiasi hicho kimeongezeka kwa Sh300 bilioni, sawa na asilimia 30, ikilinganishwa na Sh1.02 trilioni zilizokusanywa kipindi kama hicho mwaka 2025.
Amesema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, makusanyo ya gawio na michango kutoka taasisi na mashirika yanayosimamiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina yameongezeka kwa kiwango kikubwa kutoka Sh637 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia Sh1.32 trilioni mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 108.
Aidha, amebainisha kuwa kiwango kilichotangazwa hakijajumuisha mapato yaliyotolewa na baadhi ya taasisi ambazo ni Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).
Ameongeza kuwa taasisi hizo zilichangia Sh70.7 bilioni, Sh114.14 bilioni, Sh208.5 bilioni na Sh90.39 bilioni mtawalia, lakini fedha hizo hazikuhesabiwa katika jumla ya gawio la mwaka huu.
Mchechu amesema kuwa iwapo michango ya taasisi hizo ingejumuishwa kwenye hesabu za mwaka huu, jumla ya gawio na michango ambayo Serikali ingepokea ingefikia Sh1.811 trilioni.

