
Viongozi wa mjadala katika mkutano wa ngazi ya juu wa Makatibu Wakuu wa Hazina na Maafisa Waandamizi wa Benki Kuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), (kutoka kushoto) ni Mkurugenzi Mkuu Mwandamizi wa Masuala ya Uchumi kutoka Wizara ya Fedha ya Zimbabwe Mhe. Joseph Mverecha, akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu Mwandamizi na Mwenyekiti wa Maafisa Wakuu wa Hazina wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Themba Zulu, Naibu Katibu Mtendaji anayeshughulikia Ujumuishaji wa Kikanda, Sekretarieti ya SADC Bi. Angele Makombo N’tumba na Mkurugenzi wa Fedha, Uwekezaji na Forodha wa SADC. Dkt. Yolanda Sabino.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, akifuatilia na kusikiliza hoja mbalimbali zinazowasilishwa na wajumbe wakati wa Kikao cha Makatibu Wakuu wa Hazina na Maafisa Waandamizi wa Benki Kuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kinachoendelea jijini Harare, Zimbabwe.

Na Eva Ngowi, WF, Harare – Zimbabwe
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maamry Mwamba, ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Kikao cha Makatibu Wakuu wa Hazina na Maafisa Waandamizi wa Benki Kuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kinachofanyika jijini Harare, Zimbabwe, kikijadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kifedha, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda huo.
Kikao hicho kimewakutanisha Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama wa SADC, ambapo pamoja na ajenda kuu ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC, wajumbe walipitia maendeleo ya Viashiria vya vigezo vya uchumi jumla (Macroeconomic Convergence), Uimarishaji wa Masoko ya Mitaji, pamoja na maendeleo ya Mfumo wa Malipo wa Kikanda wa SADC (SADC-RTGS).
Aidha, Kikao hicho kilijadili mapendekezo ya kutumika kwa njia mbadala za kugharamia Bajeti, programu na miradi mbalimbali ya kikanda, ambazo ni kwa kutumia Tozo ya Bidhaa zinazoingia nchini kutoka Nje ya Afrika (Import Levy) na Tozo ya Utalii (Tourism Levy) ambapo nyingi zilionesha wasiwasi wao wa utekelezaji wa njia hizi kwa kuwa zinakinzana na sheria za nchi wanachama za Mamlaka za Mapato na kupunguza mapato na pia zitaongeza gharama za shughuli za Utalii na kupelekea kushuka kwa Sekta ya Utalii.
Kikao hicho pia kilijadili hatua za kuimarisha uwekezaji na maendeleo ya Mfuko wa Maendeleo wa SADC, mapitio ya utekelezaji wa maamuzi ya mikutano iliyopita, uimarishaji wa usimamizi wa sekta ya fedha, pamoja na mikakati ya kupambana na utakatishaji fedha Haramu na ufadhili wa ugaidi katika ukanda wa SADC.
Katika mjadala wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda, Tanzania imeendelea kusimamia msimamo wake wa kuunga mkono juhudi za utekezaji wa Mfuko huo, huku ikisisitiza umuhimu wa nchi wanachama kuhakikisha utekelezaji wa maamuzi na maazimio yote yanayofikiwa katika vikao vya SADC ili kuharakisha mchakato wa kusaini, kuridhia na kuanza utekelezaji wake.
Akichangia mjadala huo, Dkt. Mwamba alisema utekelezaji madhubuti wa maamuzi ya kikanda ni msingi muhimu wa kuhakikisha programu na miradi ya SADC inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Alisema ingawa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC unalenga kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, bado kuna changamoto zinazohusiana na uwezo wa nchi wanachama kuchangia, hasa kutokana na tofauti za kiuchumi na vikwazo vya kibajeti vinavyoikabili baadhi ya nchi.
“Utekelezaji wa bajeti, programu na miradi ya maendeleo ya kikanda ni muhimu kwa nchi wanachama kuendelea kutekeleza maamuzi na maelekezo yanayotokana na maazimio ya kikao na mikutano mbalimbali ya SADC ili kuharakisha mchakato wa kusaini, kuridhia na kuanza kutekeleza Mfuko huu.” Alisema Dkt. Mwamba
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uwezo halisi wa kifedha wa nchi wanachama, akieleza kuwa mchakato wa uanzishaji wa mfuko huo unapaswa kuambatana na tathmini ya kina ya uwezo wa nchi kuchangia mtaji wake, hasa katika mazingira ya ongezeko la madeni na vikwazo vya bajeti.
“Mchakato wa kutekeleza Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC unapaswa kuzingatia makadirio halisi ya uwezo wa kifedha pamoja na tathmini ya uwezo wa nchi wanachama kuchangia mtaji wa mfuko huo, hususan katika mazingira ya ongezeko la madeni na vikwazo vya kibajeti,” alifafanua Dkt. Mwamba.
Dkt. Mwamba pia alisisitiza umuhimu wa uwiano kati ya michango ya nchi wanachama na rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo, akibainisha kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda hadhi ya Mfuko, kuimarisha uendelevu wake na kuhakikisha unatimiza malengo ya maendeleo ya kikanda.
“Ni muhimu kuzingatia uwiano unaofaa kati ya michango ya nchi wanachama na rasilimali kutoka kwa washirika wa maendeleo. Hii itasaidia kuhifadhi hadhi ya mfuko, kulinda uhuru wake na kufikia vipaumbele vya maendeleo kama ilivyokusudiwa,” aliongeza.
Alihitimisha mchango wake kwa kueleza dhamira ya Tanzania katika mchakato huo, akibainisha kuwa Tanzania tayari imesaini mkataba wa kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC, na taratibu za uridhiaji zinaendelea kukamilishwa kabla ya taarifa rasmi kuwasilishwa Sekretarieti ya SADC.
Mapendekezo yanayotokana na kikao hicho yanatarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa SADC kwa ajili ya maamuzi yatakayochochea ukuaji wa uchumi, uwekezaji na ushirikiano wa kifedha katika ukanda wa Kusini mwa Afrika.
