Newala, Mtwara
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa daraja la mawe la Kanyunye na ufunguaji wa barabara yenye urefu wa kilomita 2.6 katika kijiji cha Kanyunye, wilayani Newala kumeleta suluhisho la kudumu la usafiri na usafirishaji wa mazao hususani zao la korosho linalozalishwa kwa wingi katika kijiji hicho.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea miradi inayotekelezwa na TARURA kupitia mradi wa RISE programu ya kuondoa vikwazo barabarani (Bottleneck), Meneja wa TARURA wilaya ya Newala, Mhandisi Silvester Balama amesema waliibua mradi huo kutokana na changamoto ya mawasiliano ambayo wananchi wa eneo hilo walikuwa wakikabiliana nayo.
”Wakazi wa kijiji hiki wengi ni wakulima wa zao la korosho na ghala lao la kihifadhi korosho zikishavunwa lipo katika kijiji cha Moneka kwa hiyo walikuwa wanapata shida kusafirisha mazao yao kutoka Kanyunye kwenda Moneka kwa sababu ya kukosekana kwa kivuko na barabara” ,amesema Mhandisi Balama.
Ameongeza kuwa ili mazao yao yaweze kufika katika kijiji cha Moneka ambako ndipo lilipo ghala la kihifadhia korosho ilikuwa lazima wazunguke upande mwingine katika vijiji vya wilaya ya Masasi ili waweze kulifikia ghala hilo.
”Uwepo wa kivuko hiki kumesaidia kutoa mazao moja kwa moja kutoka kijiji cha Kanyunye kwenda kijiji cha Moneka ambako kuna ghala lao. Pia kijiji cha Kanyunye hakina shule, shule yao ya msingi ipo kijiji cha Moneka, watoto walikuwa wanapata shida sana namna ya kuvuka kwenye mto huu kwa hiyo baada ya ujenzi huu imekuwa ni ukombozi mkubwa kwao kwa maana sasa watoto wanapita juu na wanawahi kufika shule”.
Bi. Zainabu Mohamedi Seif mkazi wa kijiji cha Kanyunye amesema kabla ya ujenzi wa daraja hilo walikuwa wakitembea umbali mrefu kuzifikia huduma za afya hospitali ambayo ipo mjini Newala lakini sasa hivi wanakodi bodaboda tu kwenda Newala kwa wakati na kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake, Bw. Mohamed Seif Hussein maarufu mzee Mchomolo amesema wao kama wananchi wamefurahishwa na ujenzi wa daraja hilo na kwamba limewakomboa kwa namna nyingi.
”Hii njia ilikuwa ni ya kichochoro baada ya kutengeneza barabara na kujengwa hili daraja sasa hivi imekuwa barabara maarufu ya kupita sio sisi tu bali hata wenzetu wa kijiji jirani cha Mwanona wameacha kuzunguka huko sasa hivi wanapita barabara hii kwenda Newala, kabla ya hapo tulikuwa tunateseka sana” amesema mzee Mchomola.
