Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepiga marufuku matumizi ya dawa za mifugo zenye kiambata hai cha Levamisole nchini Tanzania baada ya kufanya tathmini ya matumizi na usalama wa dawa hizo kwa mifugo na afya ya binadamu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMDA, kiambata hai cha Levamisole kimekuwa kikitumika kwenye dawa za mifugo kwa ajili ya matibabu na kinga dhidi ya minyoo, lakini tathmini imeonesha kuwepo kwa changamoto za kiafya kutokana na matumizi yake.

TMDA imeeleza kuwa kuna mwingiliano mkubwa wa kiafya kati ya binadamu na mifugo, hususan kupitia ulaji na matumizi ya mazao yanayotokana na wanyama waliotibiwa kwa dawa mbalimbali, ikiwemo dawa zenye kiambata hicho.

“Ushahidi wa kisayansi unaonesha kuwa mifugo wanapopewa Levamisole kwa kiwango kikubwa kuliko kinachotakiwa au wanapotumia kwa muda mrefu, hali hiyo inaweza kusababisha sumu ya dawa (toxicity),” imeeleza TMDA katika taarifa yake.

Kwa mujibu wa mamlaka hiyo, sumu inayotokana na matumizi ya dawa hizo inaweza kusababisha msisimko uliopitiliza wa mfumo wa neva kwa wanyama, hali inayoweza kuambatana na dalili mbalimbali ikiwemo mnyama kutoa mate mengi na povu mdomoni, kutetemeka kwa misuli, kuyumba kwa mwili, degedege, kukaza kwa misuli na hata kifo kutokana na kupooza kwa misuli ya upumuaji.

Kutokana na athari hizo na uwezekano wa kuwepo kwa mabaki ya dawa hizo kwenye vyakula vinavyotokana na wanyama, TMDA imesema imeamua kupiga marufuku dawa zote za mifugo zenye kiambata hai cha Levamisole katika soko la Tanzania.

“Tangu sasa dawa hizo hazitaruhusiwa kutengenezwa, kuingizwa nchini, kusambazwa, kuuzwa au kutumika kwa ajili ya mifugo nchini,” imeeleza TMDA.

Aidha, TMDA imewaelekeza waingizaji na wasambazaji wa dawa hizo kusitisha mara moja usambazaji wake na kuziondoa sokoni ndani ya siku 14 tangu kutolewa kwa taarifa hiyo.

Wafugaji, wafanyabiashara na wadau wengine wenye dawa hizo wametakiwa kuziwasilisha katika ofisi za TMDA za kanda zilizopo Dodoma, Arusha, Mbeya, Ruvuma, Tabora, Mwanza, Geita, Dar es Salaam na Morogoro.

TMDA imesema itaendelea kutekeleza jukumu lake la kulinda afya ya umma na viumbe hai kwa kuhakikisha dawa zote zinazopatikana nchini zinakuwa na ubora, usalama na ufanisi unaotakiwa.