Na Farida Mangube, Morogoro
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imewataka walimu nchini kuchangamkia fursa ya matumizi ya teknolojia ya Akili Unde (AI) katika ufundishaji na ujifunzaji ili kuongeza ufanisi wa kufundisha, kuboresha matokeo ya ujifunzaji na kuinua ubora wa elimu.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu wa Lugha ya Kiingereza Tanzania (TELTA) uliofanyika mkoani Morogoro, Mratibu wa EdTech kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Alcardo Alex, alisema serikali imeweka kipaumbele katika matumizi ya teknolojia zinazoibukia, hususan Akili Unde, ili kuendana na mabadiliko ya kidijitali na kuimarisha sekta ya elimu.
Alisema wizara imeandaa miongozo ya matumizi ya Akili Unde katika ngazi zote za elimu, kuanzia elimu ya awali hadi vyuo vikuu, kwa lengo la kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji, huku ikiendelea kuwajengea walimu uwezo wa kutumia teknolojia hiyo kwa ufanisi.
Aidha, alisema serikali imekamilisha madarasa janja 210 ambayo tayari yameanza kutumika, na inaendelea na mpango wa kuyasambaza katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza matumizi ya teknolojia katika shule na taasisi za elimu.
Kwa mujibu wa Dk. Alex, matumizi ya Akili Unde yatawawezesha walimu kuandaa vipindi vya masomo, kutunga na kusahihisha mitihani, kufuatilia maendeleo ya wanafunzi na kuboresha mbinu za ufundishaji.
“Ni muhimu walimu kujifunza na kutumia teknolojia ya Akili Unde kwani ni fursa ya kuongeza maarifa, kubadilishana uzoefu na kuboresha ubora wa elimu,” alisema Dk. Alex.
Akizungumza Katika atika mkutano huo, Kaimu Mkuu wa Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, Jeanne Clark, alisema walimu wa Tanzania wenye umahiri wa lugha ya Kiingereza na Kiswahili wana fursa ya kufundisha Kiswahili nchini Marekani iwapo wataendelea kuimarisha ujuzi wao wa lugha na kuendana na mabadiliko ya teknolojia.
Alisema mahitaji ya walimu wenye uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa katika ufundishaji yanaongezeka duniani, hivyo ni muhimu walimu wa Tanzania kujiendeleza ili kunufaika na fursa za kimataifa.
Kwa upande wake, Mratibu wa TELTA, Dk. Ayoub Msuya, alisema matumizi ya Akili Unde yatawasaidia walimu kuandaa masomo kwa ubora zaidi, kuboresha mbinu za kufundishia na kuwasaidia wanafunzi kuelewa lugha ya Kiingereza kwa urahisi.
Naye Mkuu wa Idara ya Taaluma za Lugha katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dk. Onesimo Nyinodi, alisema idara hiyo imepewa jukumu la kuratibu mafunzo ya matumizi ya Akili Unde kwa walimu wa lugha ya Kiingereza nchini.
Alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha walimu kutumia teknolojia hiyo kwa ufanisi katika kuboresha ufujifunzaji na matokeo ya ujifunzaji.

