NA DENIS MLOWE,IRINGA
MDAU wa maendeleo mkoani Iringa, Faraji .S.Abri amewataka vijana kuchangamkia ajira sehemu mbalimbali kwa kutumia fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ikiwemo kujitika katika ufugaji na kilimo na kutosubiri ajira za serikali.
Alisema hakuna nchi duniani ambayo inaweza kuajiri kila mmoja lakini elimu zinazotolewa pamoja na ya zinawaandaa vijana kujiajiri wenyewe hasa katika sekta za ufugaji, kilimo,na uvuvi, ambapo baadhi ya vijana ambao wamejikita katika sekta hizo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kimaisha.
Alisema kuwa vijana wanatakiwa kutambua kuwa maisha ya zamani ya vijana wa vijijini kukimbilia mijini yamebadilika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa sasa ni wakati wa vijana wa mjini kukimbilia vijijini na kujikita katika sekta zenye tija kama ufugaji wa kuku wa kisasa ambayo imekuwa mkombozi mkubwa katika ajira.
Aliongeza kuwa endapo vijana wengi wakitumia vyema sekta ya ufugaji na kilimo ni hatua ya kuunga mkono na kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya Rais Dk.John Magufuli ya hapa kazi tu na kuwa na Tanzania ya Viwanda hasa katika sekta ya kilimo.
Alisema imefika wakati vijana wa kutumia fursa hiyo ikiwa ni pamoja na kutumia ufugaji wa kuku na mifugo mingine kwa lengo la kuongeza kipato cha familia kwani kwa sasa ni moja ya biashara inayolipa ukifata misingi na nidhamu ya ufugaji.
“Mimi nilianza na vifaranga 50 nafuga kama kitoweo lakini baada ya kupata mafunzo kutoka Silverlands kusoma soma vitabu mbalimbali nikaona hii ni fursa ya kuingiza kipato na nilianza tangu mdogo na sasa nina kuku zaidi 5000 wa mayai ambao natoa trey 80 kwa siku hivyo nawasihi vijana mtumie vyema fursa hii kujikwamua kiuchumi kwani ufugaji unalipa” alisema
Faraji Abri aliongeza kuwa imefika wakati warudi na kuitekeleza kauli ya kama unataka mali utaipata shambani, ambayo itafanikiwa kwa watanzania kuwekeza kwenye shughuli za ufugaji, kilimo, na uvuvi.
Aidha aliongeza kuwa katika sekta ya ufugaji wanakumbana na changamoto ya soko kwa kuwa wengi wa wafugaji mkoani hapa hawana soko kamili ambalo watakuwa wanalitumia katika kuuza bidhaa za kuku kwa uwiano.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo amekuwa mstari wa mbele katika kuwaita wafugaji mkoani hapa wakae pamoja na kuamua soko la bidhaa za ufugaji husasani kuku ziwe ambazo zinaendana kuliko hali ilivyo sasa kila mfugaji ana bei yake.
Alisema kuwa changamoto nyingine ambayo wanakumbana nayo katika suala la ufugaji ni magonjwa ya kuku ambayo yanatagemea na mabadiliko ya hali ya hewa hivyo kusababisha hasara kwa kuku baaadhi kufa kutokana na kutokuwa na ustahimilivu wa kukabiliana na magonjwa husika ya wanyama.