Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula akizindua chanjo ya watoto kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo kiwilaya ilifanyika katika Kata ya Naberera, Kijiji cha Landanai.
Wanafunzi wa shule ya msingi Landanai Kata ya Naberera Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakiimba wimbo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika.
***********************
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, mhandisi Zephania Chaula amewataka watu wote watakaohusika na kuwatumikisha watoto chini ya miaka18 kwenye maeneo ya migodini, majumbani, machungani na kwenye biashara za mama lishe wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kukamatwa na kushtakiwa.
Mhandisi Chaula akizungumza jana kwenye kijiji cha Landanai katika maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika alisema kila mwanaume yeyote atakayehusika kumpa mimba mtoto au mwanafunzi wa kike achukuliwe hatua za kisheria na endapo mtoto hatataja mwanaume aliyehusika wazazi pamoja na mtoto wachukuliwe hatua.
Alisema mangariba wanaohusika katika kuwakeketa watoto wa kike, wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na sheria ichukue mkondo wake.
Alisema kila mtu ahakikishe anakuwa mlinzi wa mtoto kwa kushirikiana na wadau wanaohusika na masuala ya mtoto pamoja na serikali.
Alisema watoto wote wenye umri wa kwenda shule waandikishwe shule, mzazi yeyote atakaye kaidi agizo hili achukuliwe hatua za kisheri, aidha walimu wakuu wahakikishe kuwa wanafunzi wote wanavaa sare za shule (viatu na mavazi) na endapo wazazi watakwepa kuwajibika wachukuliwa hatua.
“Wazazi wahakikishe kuwa wanachangia chakula shuleni ili watoto wapate mazingira mazuri ya kujifunza, kusitisha uvamizi, uporaji na uuzaji wa ardhi ya wanachi kiholela katika maeneo ya vijiji,” alisema mhandisi Chaula.
Alisema kila kaya ihakikishe kuwa inatunza chakula cha mwaka mzima ili kuepuka janga la njaa na kila kaya ihakikishe inajiunga na bima ya afya iliyoboreshwa ili kuepuka gharama kubwa za matibabu endapo magonjwa yanapotokea na kila kijiji kihakishe kinatunza vyanzo vya maji vinavyopatikana katika maeneo yao.
Kwa upande wake, mtoto John Mollel ambaye ni mwanafunzi wa darasa la saba kweye shule ya msingi Landanai akisoma risala ya maadhimisho hayo alisema maadhimisho haya ya siku ya mtoto wa Afrika yalianza rasmi mwaka 1991.
Alisema chimbuko la siku hiyo ni kutokana na azimio la nchi 51 wanachama wa uliokuwa Umoja wa Mataifa huru ya Afrika (AU) la Juni 1991, ikiwa ni lengo la kukumbuka mauaji ya kinyama waliyofanyiwa watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini mwaka 1976.
Alisema katika azimio hilo la nchi 51 za AU, Tanzania ilijiwekea malengo mbalimbali juu ya ulinzi, haki na maendeleo ya mtoto kama vile, kupunguza idadi ya vifo vya watoto wachanga chini ya miaka 5, kupunguza vifo vya kinamama vinavyotokana na matatizo ya uzazi, kupunguza viwango vya utapiamlo miongoni mwa watoto chini ya miaka 5, kuhakikisha watoto wote waliofikia umri wa kwenda shule wanaandikishwa na kuhudhuria shule na kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto bila ubaguzi.
Alisema kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika kwa mwaka huu ni “Mtoto ni Msingi wa Taifa endelevu: Tumtunze, Tumlinde na kumwendeleza.” Kauli mbiu hii ina maanisha kuwa sisi watoto tunatakiwa tulindwe na tulelewe ipasavyo kielimu, kimwili, kiroho, kisaikolojia na kimaadili ili tuwe na msingi imara kwa maendeleo ya Taifa letu.
Hata hivyo, ofisa maendeleo ya jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Asia Ngalisoni alimhakikishia Mkuu huyo wa wilaya kutekeleza maagizo hayo yaliyotolewa naye.
Ngalisoni alisema jamii inapaswa kutambua kuwa kila mtoto wa mwenzake ni mtoto wake ili waweze kuwa na jamii yenye upendo, maendeleo na mshikamano kwa siku za baadaye.