
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya uhamisho na uteuzi wa viongozi. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka, uhamisho na uteuzi huo ni kama ifuatavyo:
(i) Dkt. Seif Abdallah Shekalaghe amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria. Dkt. Shekalaghe anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt. John Anthony Jingu ambaye aliteuliwa kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania;
(ii) Dkt. Grace Elias Magembe ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya. Dkt. Magembe alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali;
(iii) Bw. Charles Ngeleja Kadonya ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki. Bw. Kadonya anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Balozi Stephen Patrick Mbundi ambaye aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Machi 2026; na
(iv) Prof. Verdiana Grace Masanja ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).
Tarehe ya uapisho wa Makatibu Wakuu wateule itatangazwa baadaye.
