Na Sophia Kingimali.
Waajiri nchini wametakiwa kuzingatia kwa umakini wajibu wao wa kuwasilisha michango ya hifadhi ya jamii kwa wakati ili kulinda ustawi wa wafanyakazi na kuhakikisha wanapata mafao stahiki wanapostaafu.
Wito huo umetolewa leo Juni 25,2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano ya Kazi, Deus Sangu, wakati wa Mkutano Mkuu wa 67 wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), ambapo alisisitiza kuwa hifadhi ya jamii ni nguzo muhimu ya usalama wa maisha ya wafanyakazi baada ya kumaliza ajira.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu mifuko ya hifadhi ya jamii ili kuhakikisha michango ya wafanyakazi inawasilishwa kwa wakati na kwamba kila mfanyakazi ananufaika na haki zake kwa mujibu wa sheria.
Sangu amesema licha ya kuwepo kwa maoni kutoka kwa baadhi ya waajiri kuhusu viwango vya michango, tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa viwango vilivyopo vinaweza kubebwa na waajiri na wafanyakazi bila kuathiri shughuli za uzalishaji.
Ameeleza kuwa michango hiyo ndiyo msingi wa upatikanaji wa mafao ya uzeeni na huduma nyingine za kijamii, hivyo kutowasilishwa kwa wakati kunaweza kuathiri mustakabali wa wafanyakazi wengi nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amesema mfuko huo umeendelea kutoa fursa ya msamaha wa faini kwa waajiri wenye madeni ya michango ili kuwapa nafasi ya kurekebisha dosari na kurejea katika mfumo rasmi wa uchangiaji.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Wakili Suzanne Ndomba-Doran, amesema ushirikiano kati ya Serikali, waajiri na wafanyakazi utaendelea kuimarishwa ili kujenga mfumo bora wa hifadhi ya jamii unaonufaisha pande zote na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hery Mkunda, amewahimiza wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji, akisema mazingira bora ya kazi na utekelezaji wa wajibu kwa kila upande ni msingi wa kuongeza tija na maendeleo ya taifa.

