Na. Sixmund Begashe, MNRT
WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia Mfuko wa Kuhifadhi Wanyamapori Tanzania (TWPF), imekabidhi pikipiki kwa Halmashauri 22 na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMA) 11, kwa ajili ya shughuli za uhifadhi ikiwemo udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo ya vijiji nchini.
Akikabidhi pikipiki hizo, Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema pamoja na mapambano dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu, pikipiki hizo pia zitatumika katika
kurahisisha ukusanyaji wa taarifa za matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu na kuziwasilisha kwa wakati ili kurahisisha ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi kwa waathirika wa matukio hayo.
Dkt. Kijaji amesisitiza kuwa ugawaji wa pikipiki hizo ni jitihada zinazofanywa na Serikali chini ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa salama huku wakifurahia matunda ya uhifadhi wa maliasili za taifa.
Aidha, ameziagiza Halmashauri na Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori zilizokabidhiwa pikipiki hizo kuhakikisha wanazitumia vyema kulingana na malengo yake ili kuendeleza tabasamu kwa Watanzania hususani wanaoishi pembezoni mwa Hifadhi za Taifa na si vinginevyo.
Akizungumzia zoezi hilo, Mwenyekiti wa Maafisa wa Wanyamapori wa Wilaya (DGOs) Bi. Fatuma Juma, pamoja na kuipongeza Wizara kwa kuendelea kuwatambua na kuwapa ushirikiano mkubwa, amesema watatumia vitendea kazi hivyo kama walivyoelekezwa ili vitoe matokeo chanya yaliyokusudiwa.
Zoezi hilo la ugawaji wa pikipiki 22 kwa Halmashauri na 11 kwa Jumuiya za Hifadhi za Wanyamapori (WMA) lilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Nkoba Mabula, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Alexander Lobora, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa TWPF Prof. Jafari Kideghesho na viongozi wengine wa Wizara na Taasisi zake.
