Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog,Dodoma
Kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) tangu kuanzishwa kwake, Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Kupitia Mwenyekiti wake Deodatus Balile, limeipongeza hospitali hiyo kwa mafanikio makubwa ya utoaji huduma za afya, hususan huduma ya upandikizaji wa uloto.
Akizungumza Juni 25, 2026, wakati WA ziara ya kutembelea hospital hio, Balile amesema kuwa BMH imeonyesha uwezo mkubwa wa kitaalamu kwa kuwa hospitali ya kwanza kufanya huduma ya upandikizaji wa uloto na wagonjwa wote waliopatiwa huduma hiyo wamepona na wanaendelea kuishi.
Amebainish kuwa mazingira na huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo ni za kiwango cha juu, jambo linalowafanya wagonjwa kuanza kupata nafuu hata kabla ya kuonana na daktari kutokana na mapokezi na huduma bora wanazopata.
Aidha, Balile ametoa wito Kwa Watanzania kuendelea kuchangia matibabu ya wagonjwa wa selimundu (sickle cell) kupitia mifumo iliyowekwa, akisisitiza kuwa mchango wa kila mwananchi una umuhimu mkubwa katika kusaidia wagonjwa wanaohitaji huduma hizo.
Awali Akizungumza, Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dkt. Abdallah Baja, amesema kuwa hospitali hiyo ni kituo muhimu cha mafunzo kwa wanafunzi wa fani mbalimbali za afya kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na vyuo vingine nchini wanaofika kupata mafunzo kwa vitendo.
Amesema kuwa mwaka 2025 BMH ilishika nafasi ya kwanza kwa ubora wa utoaji huduma za afya miongoni mwa hospitali za rufaa za kanda nchini.
Aidha, amebainisha kuwa BMH ndiyo hospitali ya kwanza katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kufanya upandikizaji wa uloto, huku ikiwa hospitali ya pili nchini kufanya upandikizaji wa figo baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Dk. Baja ameongeza kuwa BMH pia ni hospitali ya kwanza nchini kufanya upandikizaji wa uume (penile transplant), huduma inayosaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazohusiana na afya ya mfumo wa uzazi wa mwanaume.
Kilele cha maadhimisho ya miaka 10 ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kinatarajiwa kufanyika Julai 15, 2026 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

