NA DENIS MLOWE, IRINGA 
WATENDAJI wa vijiji, viongozi wa serikali za mitaa na wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Iringa wamepatiwa mafunzo na uelewa kuhusu utekelezaji wa Mradi wa INUA II unaotekelezwa na Hand in Hand Eastern Africa Tanzania (HIHEA), ukiwa na lengo la kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia shughuli za uzalishaji na biashara.
Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Hand in Hand Eastern Africa Tanzania, Jane Richard Sabuni, alisema taasisi hiyo imefungua rasmi ofisi yake mkoani Iringa na kuanza utekelezaji wa mradi huo unaolenga kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato kupitia vikundi vya ujasiriamali na biashara mbalimbali.
Alisema Hand in Hand imejikita katika kusaidia wananchi kuanzisha na kukuza biashara halali zitakazochangia kuimarisha uchumi wa kaya na kuboresha maisha ya familia, huku ikiweka mkazo katika ushirikiano wa wanajamii na viongozi wa maeneo husika.
“Tunajiona kama daktari wa pochi za wananchi tunataka kuona wananchi wanapata maarifa, wanaanzisha biashara na kuongeza kipato ili kuboresha maisha yao na ya familia zao,” alisema Sabuni.
Alieleza kuwa Mkoa wa Iringa ni wa saba kufikiwa na taasisi hiyo baada ya kutekeleza miradi yake katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma na Simiyu, huku mipango ikiendelea ya kupanua shughuli zake katika mikoa mingine ikiwemo Njombe na Tabora ndani ya miaka mitano ijayo.
Sabuni alisema kuwa Hand in Hand Tanzania imefanikiwa kuwafikia zaidi ya wananchi 87,000 kupitia programu zake mbalimbali, kusaidia kuanzishwa kwa biashara zaidi ya 50,000 na kuchangia kuzalishwa kwa ajira zaidi ya 74,000 kupitia vikundi zaidi ya 4,000 vya kiuchumi vilivyoundwa na kuimarishwa.
Alibainisha kuwa semina hiyo imeandaliwa mahsusi kuwajengea uwezo viongozi wa serikali za vijiji na kata ili waweze kuelewa malengo ya mradi, walengwa wanaotarajiwa kunufaika na nafasi yao katika kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo zitakazotekelezwa.
Sabuni alisisitiza kuwa ushirikiano wa viongozi wa serikali za mitaa ni nguzo muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Mradi wa INUA 2 akitoa wito kwa watendaji na wenyeviti wa vijiji kushirikiana kwa karibu na taasisi hiyo ili kuhakikisha fursa zinazotolewa zinawafikia wananchi wengi zaidi.
Naye Mratibu wa Programu wa Hand in Hand Eastern Africa Tanzania, Matthew Allen, alisema lengo la mkutano huo ni kuwashirikisha viongozi wa kata na maafisa maendeleo katika hatua za awali za utekelezaji wa mradi ili waweze kuufahamu kwa undani na kushiriki katika kuwafikia walengwa.
Alisema mradi huo unalenga kuwafikia wananchi wanaoishi katika mazingira ya umaskini kupitia mfumo wa ushirikiano na viongozi wa maeneo husika, ambao watakuwa kiungo muhimu kati ya taasisi hiyo na jamii.
“Jana tulianzia ngazi ya mkoa, leo tupo ngazi ya wilaya kwa kuwashirikisha watendaji wa kata na maafisa maendeleo ili waweze kuuelewa mradi wetu na namna tutakavyoshirikiana katika kuwafikia walengwa tunataka viongozi hawa wawe sehemu ya mchakato mzima wa utekelezaji wa mradi katika ngazi ya jamii,” alisema Allen.
Na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Dora Mlomo, alisema mradi huo una tofauti na miradi mingi iliyopita kwa kuwa unaweka mkazo mkubwa katika utoaji wa elimu na kujenga uwezo wa wanufaika kabla ya kuanza shughuli za uzalishaji na biashara.
Alisema mafunzo yatakayokuwa yakitolewa yatawasaidia wanufaika kupata maarifa ya kina kulingana na shughuli wanazokusudia kufanya, ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara pamoja na usimamizi wa fedha.
“Tunauona mradi huu kuwa na manufaa makubwa kwa jamii kwa sababu utaanza kwa kujenga uwezo wa wananchi. Wanufaika watafundishwa elimu ya fedha, utunzaji wa kumbukumbu za biashara, utafutaji wa masoko na pia wataunganishwa na wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani kulingana na shughuli wanazofanya,” alisema Mlomo.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Ruaha, Fuad Mwasiposya, alisema mradi huo umefika kwa wakati muafaka kwani unakwenda kuziba pengo la elimu ambalo limekuwa likikwamisha juhudi mbalimbali za kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Alisema pamoja na kuwepo kwa mikopo inayotolewa na serikali na taasisi za fedha, wananchi wengi wamekuwa wakikosa maarifa ya usimamizi wa fedha na biashara jambo linalopelekea baadhi yao kushindwa kutumia kikamilifu fursa hizo.
“Mradi huu umekuja na suluhisho la changamoto ambayo tumekuwa tukikabiliana nayo kwa muda mrefu. Watu wengi wanapata mikopo lakini hawana elimu ya kutosha kuhusu biashara na usimamizi wa fedha. Hand in Hand wamekuja kujibu swali hilo kwa kutoa mafunzo yatakayowasaidia wananchi kugeuza mawazo yao kuwa miradi yenye tija,” alisema Mwasiposya.
Mradi wa INUA II unatarajiwa kutekelezwa katika kata 13 za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ukiwa na lengo la kuongeza uwezo wa wananchi kujiajiri, kukuza biashara ndogo na za kati, pamoja na kuchangia kupunguza umaskini kupitia uwezeshaji wa kiuchumi katika ngazi ya jamii.